Mbelgiji wa Yanga kicheko, Z'bar vilio

11Jan 2020
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Mbelgiji wa Yanga kicheko, Z'bar vilio
  • ***Mashabiki walia kuikosa dabi, kocha huyo mpya aonyesha kukunwa na pasi za kasi pamoja na...

AKIISHUHUDIA jukwaani kwa mara ya kwanza Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, alionekana kufurahia namna wachezaji wa timu hiyo walivyokuwa wakimiliki mpira katika kipindi cha kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.

Eymael aliyetua nchini juzi na kuunganisha moja kwa moja visiwani hapa kutambulishwa kwa wachezaji, anarithi mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera aliyetimuliwa hivi karibuni.

Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa juzi usiku, Nipashe lilikuwa likimfuatilia Eymael jukwaani akiwa na wenyeji wake viongozi wa Yanga na mara kadhaa alionyesha kufurahi pindi timu hiyo ilipomiliki mpira na kuonana kwa pasi.

Yanga ilionyesha mchezo mzuri kwa kucheza pasi za haraka haraka tofauti na mchezo uliopita dhidi ya Jamhuri ambao walishinda 2-0, na dakika ya 36 ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Deus Kaseke.

Kuingia kwa bao hilo kuliongeza kujiamini kwa wachezaji wa Yanga na kuonyesha soka la kuvutia zaidi ambalo mara kadhaa lilimfanya Mbelgiji huyo kutabasamu.

Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 90 kufuatia Shomari Kibwana kuisawazishia Mtibwa Sugar na hatimaye mikwaju ya penalti kuchukua hatua yake na Yanga kutolewa katika michuano hiyo kwa kufungwa matuta 4-2.

Kutolewa kwa Yanga kulizua 'vilio' na huzuni kubwa kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakitamani itinge fainali sambamba na Simba ili washuhudie 'dabi' ya watani hao wa jadi.

"Tumeikosa dabi ya watani, hii Yanga imetupunguzia utamu wa Mapinduzi, wangepita na Simba kesho (jana usiku), tungeburudika sana,” alisema shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Maulid Abdullah.

Aidha, mjumbe mmoja wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, aliliambia Nipashe kuwa kama ingetokea miamba hiyo kukutana ingeongeza mapato pia.

Kocha msaidizi wa Yanga, Said Maulid 'SMG' akizungumzia mchezo huo, alisema walijitahidi kupambana hadi mwisho lakini penalti hazina mwenyewe.

"Wapo wanaosema tumefanya makusudi ili kuikwepa Simba, hiyo si kweli kila mtu ameona namna tulivyopambana na kufika hatua ya penalti ambazo hazina mwenyewe," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Katika mechi hiyo ya juzi, Kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili alipangua penalti ya kiungo Abdulhalim Humud, hata hivyo, beki Kelvin Yondani aligongesha mlingoti na kiungo Abdul-Aziz Makame akapaisha juu ya lango.

Wafungaji wa penalti za Mtibwa Sugar walikuwa ni Omary Sultan, Dickson Job, Jaffary Kibaya na Shomari Kibwana na za Yanga zilifungwa na Paul Godfrey ‘Boxer’ na kiungo Mapinduzi Balama.

Habari Kubwa