Mbio za magari Iringa kuanza leo

12May 2018
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Mbio za magari Iringa kuanza leo

MADEREVA 19 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania wanatarajia kushiriki mashindano ya mbio za magari  yanayoanza leo mkoani hapa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari,  Mwenyekiti Kamati ya mashindano hayo, Amjad Khan, alisema kuwa mashindano hayo yajulikanayo kama 'Rally of Iringa' yamedhaminiwa na maji ya kunywa ya Mkwawa (Mkwawa Superior pure drinking water).

Khan alisema mashindano hayo kwa mwaka huu yatakuwa yanapita njia za mashambani kwa sababu za usalama wa wananchi na mali zao.

"Mashindano haya yatakuwa na njia tatu ambapo yataanzia katika kiwanda cha maji cha Mkwawa kilichopo Manispaa ya Iringa, na kuelekea uwanja wa CCM wa Samora baadae kupita Tanesco ya zamani hadi kijiji cha Kalenga, Nzihi na Zimamoto ambavyo vipo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Kwa upande wake Kaimu mkuu wa trafiki mkoa wa Iringa (RTO),  Isa Milanzi, aliwatahadharisha watembea kwa miguu na wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini barabarani wakati wote wa mashindano.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Hidaya Kamanga, alisema kuwa  washiriki mwaka huu wameongezeka hadi kufikia 19 tofauti na mwaka jana ambao walikuwa 12.

 "Mwaka jana walishiriki 12 lakini mwaka huu wameongezeka na kufikia 19 na tunategemea wataendelea kuongezeka kabla ya mashindano kuanza"alisema Kamanga.

Aliwataja wadhamini wa mashindano hayo kwa mwaka huu kuwa ni Famari store,Ymk Garage, Sun set Hotel, Planet 2000 pamoja vyombo mbalimbali vya usalama mkoani Iringa.