Mbio za magari kufanyika Iringa

20Jul 2019
Friday Simbaya
IRINGA
Nipashe
Mbio za magari kufanyika Iringa

MADEREVA 17 kutoka sehemu mbalimbali wamethibitisha kushiriki katika mashindano ya mbio za magari za Mkwawa (Mkwawa Rally 2019), ambazo zimepangwa kufanyika leo na kesho mkoani hapa, imeelezwa.

Mbio hizo zimeandaliwa na Klabu ya Michezo ya Magari ya Iringa (IMSC) na kudhaminiwa na kampuni mbalimbali huku wazalishaji wa Maji ya Mkwawa wakiwa ndio wadhamini wakuu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Amjad Khan, alisema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika na wanatarajia madereva wote waliothibitisha kushiriki mbio hizo watatimiza ndoto zao.

Khan alisema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwahamasisha vijana na kupenda michezo na hasa mbio za magari na vile vile kutumia michuano hiyo kuutangaza Mkoa wa Iringa.

Naye Mwakilishi wa Maji ya Mkwawa, Maria Mhina, alisema wameendelea kuudhamini mchezo huo kwa mwaka watatu mfululizo ili kuendelea kuwahamasisha vijana na watu wengine kupenda michezo hasa mbio za magari.

Mhina alisema kuwa wanawaomba wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi leo na kesho kushuhudia madevera wanavyochuana katika mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka.