Mbio za NBC Marathon zazinduliwa rasmi Dar

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mbio za NBC Marathon zazinduliwa rasmi Dar

HATIMAYE Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Shirikisho la Riadha Taifa (RT), wamezindua rasmi mbio zinazofahamika kwa jina NBC Marathon, zinazotarajiwa kufanyika Novemba 22, mwaka huu jijini Dodoma.

Pamoja na kukuza mchezo huo nchini,  mbio hizo pia zinalenga kuchochea mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi nchini, kwa mujibu wa waandaji hao.

Hafla ya uzinduzi wa mbio hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa mchezo huo wakiwamo viongozi waaandamizi wa Baraza la michezo Tanzania (BMT), Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), maofisa waandamizi wa benki ya NBC pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, alisema pamoja na dhamira yao ya dhati ya kuwekeza kwenye mchezo wa riadha kupitia mbio hizo, mapato yote yatokanayo na usajili wa wawakimbiaji yataelekezwa kwenye vita dhidi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

“Tumeamua kuelekeza nguvu zetu katika mapambano hayo tukitambua kwamba ugonjwa huu ndio unaoongoza kwa vifo vya saratani hapa nchini. Hivyo, mbio hizi za NBC Dodoma Marathon zitakuwa jukwaa zuri la kusambaza ufahamu juu ya ugonjwa huu ambao tunaambiwa kwamba ukiwahiwa unatibika,’’ alisema.

Katika hafla hiyo pia ilishuhudiwa benki hiyo pamoja na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) wakisaini mkataba  wenye thamani ya Sh. milioni 300 ikiwa ni ufadhili wa benki hiyo katika ya kuendesha mbio hizo katika kipindi cha miaka mitano.

“Ni maono yetu kwamba NBC Dodoma Marathon ndio mbio ambazo zitapeperusha jina la NBC katika miaka ijayo, na hivyo tunadhamiria kuendelea na mbio hizi kwa kipindi cha miaka mitano.”

“Zaidi ni matumaini yetu kwamba uwekezaji wetu kwenye mchezo wa riadha utatumika vizuri na hivyo kuleta mafanikio kwa wanariadha wetu na kwa nchi yetu kwa ujumla katika siku za usoni,” Sabi aliongeza kuwa usajili wa mbio hizo tayari umeanza kupitia matawi ya benki hiyo kote nchini sambamba na mitandao ya kijamii ya benki hiyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa RT, Anthony Mtaka, pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuamua kuwekeza kwenye kuinua mchezo huo nchini, alisema lengo ni kuzifanya mbio hizo kuwa za mfano na zenye utambuzi wa kimataifa (International Recognition).

“NBC Dodoma Marathon zitakuwa za  Km. 5, Km. 10, Km. 21 na Km.42, kwa kuwa lengo ni kuzifanya zitambulike kimataifa, tumehakikisha kwamba njia zote zinapimwa na mpimaji anayetambulika na Shrikisho la Riadha la Dunia (World Athletics). Zoezi hilo la kupima lilikamilika Oktoba 17, mwaka huu jijini Dodoma. Kwa sasa tunasubiri vyeti kutoka Shrikisho la Riadha la Dunia kuthibitisha utambuzi huo,’’ alibainisha.

Alisema uamuzi wa mbio hizo kufanyika jijini Dodoma ulizingatia sababu za msingi kadhaa ikiwamo mandhari ambayo ni kivutio kwa wakimbiaji, mpangilio wa barabara ambazo haziingiliani na barabara kuu na hivyo kuwa salama kwa wakimbiaji wa aina zote.

“Lakini pia tuliona Jiji la Dodoma, kama mji wetu mkuu, unastahili kuwa na tukio kubwa la mchezo unaotambulika kimataifa. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba uamuzi wetu wa kupeleka mbio hizi Dodoma ulikuwa sahihi,” alisema.

Habari Kubwa