Mechi chungu Yanga Ligi Kuu

04Jul 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mechi chungu Yanga Ligi Kuu
  • Ilianzia katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Ruvu Shooting, sare ziliwaandama huku Zahera akichelewa...

KWA mara ya tatu, Yanga imekosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kushuhudia taji hilo likienda kwa watani zao, Simba, huku sababu kubwa msimu huu ikionekana ni kukosa maandalizi ya mwanzo wa msimu, kutofanya vema mechi za mwanzo na kupata sare nyingi zilizovunja rekodi.

Kutoshinda mechi mbili za mwanzo tu, zilitosha kabisa kuifanya Yanga kuanza kuondoka taratibu kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa msimu huu wa 2019/20, hasa ikizingatiwa Simba walishinda mechi hizo za mwanzo.

Yanga ilifungua msimu kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting hapo Agosti 26, mwaka jana huu na Oktoba 3, ilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mechi hizi mbili tu, ziliifanya Yanga kubaki na pointi moja tu, huku Simba ikiwa tayari imeshakusanya pointi sita kwa kuifunga JKT Tanzania mabao 3-1 kwenye mechi ya kwanza waliyocheza Agosti 29, mwaka jana na pia kuitwanga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Septemba 13, mwaka jana.

Hii ilitokana na wachezaji wa timu hiyo kutofanya vizuri maandalizi ya kuanza kwa msimu maarufu kama 'Pre-season' iliyokuwa mjini Morogoro ikisimamiwa kwa muda mrefu wa Kocha Msaidizi, Noel Mwandila, huku Kocha Mkuu Mkongomani, Mwinyi Zahera akiwa nchini Ufaransa kwa mapumziko.

Hili ndilo linaonekana tatizo kubwa la msingi, kwani hata aliporejea, ilibaki wiki moja tu kabla ya michuano ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia Ligi Kuu Bara ikiwa imekaribia.

Zahera alionekana kutokuwa tena na muda wa kuwaandaa wachezaji, bali ni kuwapa mazoezi ya kawaida tu kwa ajili ya michuano iliyokuwa imekaribia.

Sababu nyingine ya Yanga kuukosa ubingwa msimu huu ni sare zilizopitiliza. Kwa mara ya kwanza tangu mfumo mpya wa Ligi Kuu Bara uanze msimu wa 2007/08, Yanga haijawahi kufikisha idadi kubwa ya sare kama msimu huu.

Kabla ya hata msimu haujamalizika, ikiwa imebakisha mechi sita, tayari Yanga ina sare 12 ambazo ni rekodi ya klabu.

Mara ya mwisho Yanga kupata sare nyingi kwa msimu mmoja, ilikuwa ni msimu wa 2017/18, ilipopata sare 10, na hata msimu uliopita ambapo ilionekana timu ni dhaifu zaidi chini ya Zahera, ilitoa sare tano tu.

Wakati Yanga ikiwa na idadi hiyo, Simba imetoa sare nne tu mpaka sasa. Hizo ni idadi ya sare ambazo Yanga ilitoka mfululizo msimu huu dhidi ya Mbeya City bao 1-1, sare ya bila kufungana dhidi ya Prisons, ikatoka sare tena ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania na suluhu nyingine dhidi ya Coastal Union.

Hata Simba ilipokuwa ikipoteza mechi zake hizo chache, Yanga yenyewe ilikuwa ikitoa sare na ilipokuwa ikishinda, bado Yanga iliendelea na sare zake au kufungwa.

Kutokuwa na mwendelezo mzuri wa mechi za ushindi pia kumekuwa msaada mkubwa kuinyima Yanga ubingwa msimu huu, kwani haikuwa ikishinda mechi nyingi mfululizo kama watani zao wa jadi, Simba.

Mechi nyingi mfululizo ambazo Yanga imeshinda ni tano tu, lakini baada ya hapo inacheza mechi mbili, inatoka sare, au mechi nne, inafungwa.

Wakati ikisuasua, Simba imeshinda mechi sita mfululizo mara mbili. Ilishinda mechi sita, ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC, lakini ikashinda tena mechi sita mfululizo, ndipo ikapoteza dhidi ya Yanga kwa bao 1-0.

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa Namungo kuwaalika JKT Tanzania wakati Kagera Sugar itacheza dhidi ya Ruvu Shooting huku Singida United ikiwafuata Azam FC, KMC wao watapambana na Mwadui FC na Mbao watawakaribisha Lipuli.

Kwenye Uwanja wa CCM Sokoine wenyeji Tanzania Prisons watawaalika Polisi Tanzania huku kesho Ndanda ikicheza dhidi ya mabingwa, Simba na Biashara United itawakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Habari Kubwa