'Mechi ya vigogo ngumu zaidi ya Uchaguzi Mkuu'

19Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
'Mechi ya vigogo ngumu zaidi ya Uchaguzi Mkuu'
  • ***Kocha wa Jangwani adai kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka jana ulikuwa rahisi kulinganisha na itakavyokuwa mechi ya Simba na Yanga kesho...

KOCHA wa Yanga, Hans van der amekuwa siyo mzungumzaji kuelekea mechi dhidi ya Simba, lakini jana alifunguka na kudai mchezo huo vigogo utakuwa ngumu kuliko hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliompeleka Ikulu Rais John Magufuli.

Wachezaji wa Simba na Yanga wakipambana katika moja ya mechi za ligi kuu ya Vodacom

Yanga atakuwa mwenyeji wa Simba katika mechi ya marudiano Ligi Kuu Bara kesho kwenye Uwanja wa Taifa.

Kinachoifanya mechi hiyo kubeba utabiri mgumu ni viwango vizuri dimbani kwa wachezaji wa timu zote.

Alipoulizwa kuhusu mechi hiyo, Pluijm alidai kwa kifupi: "Mechi ya Simba na Yanga safari hii ni ngumu zaidi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliopita."
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja amekuwa mzungumzaji kuelekea mechi hiyo itakayochezeshwa na refa mwanamke, ikiwa ni mara ya kwanza baina ya timu hizo Ligi Kuu Bara.

Mayanja alisema jana wakati akizungumza na gazeti hili: "Kama wachezaji watafuata kwa usahihi mbinu nilizowapa, tuna nafasi kubwa ya kufanya vuzuri.

"Ni mechi ya ushindani inayowataka wachezaji wote kuwa makini tangu mwanzo wa mchezo hadi mwisho.

PEMBA

Kambi ya Yanga iliyoko Pemba imeendelea kugubikwa na usiri kuanzia viongozi hadi wachezaji.

Katika kudhihirisha kwamba mechi ya kesho wanahitaji kushinda, wachezaji wa Yanga tangu walipotua nchini wakitokea Mauritius, hawaonekani kwenye mitandao ya kijamii na kila wanachokifanya kuwa siri.

Jana asubuhi timu hiyo haikufanya mazoezi, lakini jioni ilishusha kikosi chake chote kwenye Uwanja wa Gombani kwa ajili ya kujifua kujiandaa na mtanange huo.

"Hawaruhusu kuongea au kumsogelea mchezaji, hata salamu na wachezaji tunapeana kwa mbalimbali, si unajua mechi hii, kila mtu anaogopa kuangushiwa jumba bovu (lawama)," kiongozi mmoja wa klabu hiyo.

MOROGORO

Mbali na viongozi wakijipanga kutoa ahadi, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wanachangishana fedha ili kuwapa ahadi 'kununua' kila goli litakalofungwa katika mchezo wa kesho.

Katika kuhakikisha wanaongeza hamasa, viongozi wa timu hiyo juzi walikwenda Morogoro kuzungumza na wachezaji.
Simba inatarajia kurejea jijini leo mchana, lakini uamuzi wa hoteli ipi wachezaji wake watafikia bado haijawekwa wazi.