Messi avunja rekodi ya Pele

11Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Messi avunja rekodi ya Pele
  • ***Niliota kuhusu hili siku moja na shukrani kwa Mungu mambo yamekuwa sawa...

LIONEL Messi ameipiku rekodi ya Pele kama mfungaji mwenye mabao mengi zaidi kwa bara la Amerika Kusini kwa kufunga ‘hat-trick’ wakati Argentina ikiibuka na ushindi dhidi ya Bolivia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, juzi.

Akifunga mabao yote kwenye ushindi wa 3-0 mjini Buenos Aires, kumemfanya Messi kufikisha mabao 79 aliyoifungia Argentina katika mechi 153.

Gwiji wa Brazil, Pele alimaliza kipindi chake cha uchezaji kwa kufunga mabao 77 katika mechi 92.

Bao la kwanza la Messi dakika ya 14 likamfanya kufikia rekodi ya Pele na kisha akaivunja kipindi cha pili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alifunga bao la pili kwa kumpiga chenga mlinzi na kisha kukamilisha hat-trick dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika.

Baada ya mchezo, nahodha huyo wa Argentina, Messi na wachezaji wenzake walisherehekea wakiwa na Kombe la Copa America mbele ya mashabiki 20,000 kwenye Uwanja wa Monumental.

Alikiongoza kikosi hicho kwenye taji lake la kwanza la kimataifa Julai wakati walipoifunga Brazil kwenye fainali.

"Niliota kuhusu hili siku moja na shukrani kwa Mungu mambo yamekuwa sawa," aliandika Messi kwenye ukurasa wake wa Instagram akiweka picha ya kombe hilo.

"Sina maneno mengi ya kuzungumza, asanteni sana wote kwa mapenzi mliyoonyesha. Ulikuwa usiku mzuri, nimefurahia sana, na nimefurahia sana."

Habari Kubwa