Mexime afikiria kuimaliza Yanga

22Sep 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mexime afikiria kuimaliza Yanga

HUKU Kocha wa timu ya Kagera Sugar, Mecky Mexime, akisema kuwa kichapo cha mabao 2-0 alichopata kutoka kwa Mtibwa Sugar wiki iliyopita ni sehemu ya 'majeraha' ya soka, ameahidi kuwa anajiimarisha kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi zinazofuata

Akizungumza na gazeti hili jana, Mexime, alisema kuwa timu yake si mbaya ila wapinzani wao Mtibwa Sugar walitumia vizuri nafasi mbili walizopata katika mechi yao na kuondoka na ushindi huo muhimu.

Mexime alisema kwamba ligi bado 'haijafika penyewe' na anakiamini kikosi chake bado kina nafasi ya kupata ushindi pale atakapokutana na Yanga au Azam FC kwenye mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

"Yaani walituwahi katika dakika nne za kwanza, walipata nafasi na kufunga mabao, baadaye tulipoanza kutawala mchezo hatukufanikiwa kufunga, ila tutaamka na kuzinduka kwa hao hao vigogo waliobakia, hasa tunajipanga kukutana na Yanga, hatutaki kupoteza tena pointi Dar es Salaam," alisema nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars.

Alisema kuwa kikosi chake tayari kimeshatua Dar es Salaam na kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama kwa ajili ya kujiweka sawa kuwakabili wenyeji wao African Lyon katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru.

Katika msimamo wa ligi, Mtibwa Sugar yenye pointi tisa iko katika nafasi ya tano baada ya kushinda mechi tatu na kupoteza mbili, nyingine ikiwa ni dhidi ya Simba ambayo pia walifungwa mabao 2-0.

Habari Kubwa