Mgunda aelekeza hesabu kwa Azam FC

14Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mgunda aelekeza hesabu kwa Azam FC

KOCHA Mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda, amesema mikakati yake kwa sasa ni kupambana na Azam FC kuhakikisha katika mechi yao ya Jumamosi anaondoka na pointi tatu ili kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Coastal tayari ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Uhuru Jumamosi, wakati huu ikiwa nafasi ya tano na alama zake 35 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikizidiwa pointi tisa na Azam FC iliyopo nafasi ya pili baada ya timu hizo kila moja kushuka dimbani mara 21 hadi sasa.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Mgunda alisema baada ya kutoka suluhu ya bila kufunga dhidi ya KMC, sasa wanajipanga vizuri kwa mchezo wao ujao dhidi ya Azam ili kupata matokeo mazuri.

Alisema upungufu walioubaini zaidi ni katika safu yake ya ushambuliaji kutokuwa makini na utulivu wanapofika ndani ya 18 hali ambayo imewasababishia kukosa pointi tatu katika mchezo wao uliopita.

“Kwa sasa tunasahau matokeo ya KMC na kuanza mikakati ya kupambana na Azam, natumia siku mbili hizi kufanyia kazi upungufu huo, usijirudie katika mchezo unaofuata ili kupata pointi,” alisema.

“Tunatambua mechi dhidi ya Azam itakuwa ya ushindani, ila watambue tumekuja Dar es Salaam kutafuta pointi, hiyo inawalazimu washambuliaji wetu kuwa makini katika nafasi tunazozipata kufunga,” alisema Mgunda.

Alisema hawako katika nafasi mbaya ila anahitaji kupata pointi muhimu katika michezo yao ya ugenini na nyumbani ili kupanda hadi katika nafasi nne za juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Coastal inazidiwa alama moja na Namungo FC iliyopo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo inayotarajiwa kuendelea Jumamosi katika viwanja tisa nchini.

Habari Kubwa