Mgunda afunguka KMC 'iliwakamata'

16Oct 2020
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mgunda afunguka KMC 'iliwakamata'

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, amesema timu yake 'ilikamatika vilivyo' katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC, huku pia wachezaji wake wakishindwa kutumia vyema nafasi walizozipata.

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda.

Kauli hiyo ya Mgunda ilikuja baada ya kutoka sare ya bila ya kufungana huku timu yake pia ikikosa penalti baada ya kipa mkongwe wa KMC, Juma Kaseja kuipangua.

Mgunda alisema mchezo huo ulikuwa mzuri na timu yake ilitawala kwa kiasi kikubwa kuliko wapinzani wao, lakini tatizo la wachezaji wake lilikuwa ni umaliziaji mbovu.

"Tuliishika kabisa mechi, lakini utulivu wa wachezaji wangu kumalizia kufunga ndiyo ilikuwa tatizo, hivyo mimi kama mwalimu sichoki, siku zote mimi kwangu mwalimu wa mwalimu ni mechi, kwa hiyo mwalimu wangu wa mechi ya leo (juzi), amenionyesha mengi, nilichojifunza ni kwamba tunatengeneza nafasi nyingi, ambazo hatuzitumii," alisema Mgunda.

Katika mechi hiyo, Coastal Union italazimika kujilaumu yenyewe baada ya kukosa penalti dakika ya 43, huku pia wapinzani wao wakicheza pungufu katika kipindi chote cha pili kutokana na mchezaji wao, Ally Ramadhani kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kwa matokeo hayo, Coastal Union ilifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi sita, ikishinda moja, sare mbili na kupoteza michezo mitatu na kabla ya mechi za jana, ilikuwa katika nafasi ya 13, kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari Kubwa