Mgunda afunguka yuko hatihati kubakia Coastal

30Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mgunda afunguka yuko hatihati kubakia Coastal

LICHA ya kuibakisha Coastal Union kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Juma Mgunda ni wazi hajui hatima yake ndani ya timu hiyo ya jijini Tanga.

Juma Mgunda.

Mgunda aliliambia gazeti hili anatarajia kumaliza mkataba wake ifikapo mwezi ujao, na bado hakuna mazungumzo mapya ambayo yameshafanyika na mabosi wa timu hiyo.

Kocha huyo alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kwa sababu bado ni kocha wa timu hiyo, huku leo akitarajia pia kukabidhi ripoti ya ufundi kwa mabosi wake.

"Ni kweli mkataba wangu unaelekea mwisho. Utamalizika mwezi ujao na hili ni jambo la kawaida kwa kocha yoyote yule. Kama watanihitaji sawa, lakini kama hawanitaki, basi tutapeana mkono wa kwaheri, lakini mpaka muda huu mimi ni kocha wa Coastal Union na muda ukifika ndiyo tutaongea," alisema straika huyo wa zamani wa timu hiyo.

Aliongeza kuwa yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha ripoti ya ufundi baada ya kutumia muda mrefu wa kuiandaa.

"Huwezi kuandika ripoti ya mwaka mzima kifupi tu kama unaandika barua ya uchumba, ni lazima ukae uangalie vitu vingi vya kuainisha. Uandike vitu ambayo vitaisaidia klabu na timu yenyewe kwa ujumla na inayojitosheleza," Mgunda alisema.

Aliongeza atawasilisha ripoti ambayo itaeleza ni kwa nini Coastal Union ilifika hapo ilipo na nini kifanyike ili hali hiyo isijirudie tena msimu ujao.

"Nimeandika mazuri ya timu na mapungufu na nini cha kufanya," Mgunda alibainisha.

Coastal Union iliponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliomalizika, baada ya kuangukia katika mechi za mchujo kwa kuifunga Pamba FC ya jijini Mwanza jumla ya ambao 5-3, ikitoka sare ya mabao 2-2 ugenini kwenye Uwanja wa Nyamagana na kushinda magoli 3-1 nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani.

Timu nyingine iliyonusurika na janga la kushuka daraja na kucheza mechi za mchujo ni Mtibwa Sugar ya Morogoro, ambayo iliwaondoka Transit Camp ya jijini Dar es Salaam ambayo imebakia kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuwa na timu 16, wakati klabu zilizoshuka daraja moja kwa moja ni pamoja na Mwadui FC, Ihefu SC, Gwambina FC na JKT Tanzania.

Habari Kubwa