Mgunda alia na wachezaji kupigwa wiki

23Nov 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mgunda alia na wachezaji kupigwa wiki

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, amesema kufungwa mabao 7-0 dhidi ya Simba kumetokana na uzembe wa wachezaji wake kufanya makosa yanayojirudia.

Akizungumza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha baada ya mechi hiyo ya juzi, Mgunda alisema mabao yote ambayo Simba wameyapata kwenye mchezo huo, yanatokana na wachezaji wake kufanya makosa yanayojirudia na wenzao wakawa wepesi wa kuyatumia na kuyageuza kuwa magoli.

"Nakubali matokeo, tumefanya uzembe wenyewe. Tumefungwa mabao mepesi kwa uzembe wetu wenyewe. Kuna watu wananiambia kuwa nisingefunguka, tatizo siyo kufunguka wala kufunga, magoli tuliyofungwa si kwamba tulizidiwa sana, tunafanya makosa ya kujirudia na kwa kiwango cha wachezaji kama wa Simba ni lazima wakuadhibu," alisema.

Mgunda, straika wa zamani wa timu hiyo, alisema kuwa angalau kipindi cha pili, wachezaji wake walijirekebisha na hii ni baada ya maelekezo ya kipindi cha pili.

"Tulichojifunza ni kwamba tukifanya makosa tutaadhibiwa. Na kwa hili lililotokea hata tukianza kujadiliana hadi kesho hatutapata muafaka, mechi imeisha na cha kufanya ni kuangalia mechi inayofuata," alisema.

Baada ya kipigo hicho, Coastal inakamata nafasi ya 13, ikiwa na pointi 12 kwa mechi 11 ambazo imecheza wakati huu kesho ikiikaribisha Ihefu kwenye uwanja huo huo wa Sheikh Amri Abeid.

Habari Kubwa