Michango Serengeti Boys yaanza rasmi

17Mar 2017
Halfani Chusi
Dar es Salaam
Nipashe
Michango Serengeti Boys yaanza rasmi

WASANII Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' na Ali Kiba wanatarajia kutunga nyimbo maalum kwa ajili ya kuhamasisha wadau mbalimbali wa hapa nchini kuichangia timu ya soka ya Taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imeelezwa jana.

Mjumbe wa Kamati ya Uhamasishaji, Maulid Kitenge, alisema jana kuwa tayari wameshatayarisha midundo ambayo itatumika kwenye nyimbo hizo mpya zitakazotungwa na nyota hao pamoja na wasanii wengine.

“Tumeshaandaa 'biti' na tumeshawapatia wasanii wetu Diamond Platnumz, Ali Kiba na wasanii wengine wengi ili kutungia nyimbo zitakazosaidia kuhamasisha vijana wetu," alisema Kitenge.

Pia wito umetolewa kwa wadau wa michezo, serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kujitokeza kuichangia Serengeti Boys, katika kufanikisha safari ya kwenda kushiriki fainali za Afrika za vijana zitakazofanyika Mei nchini Gaboni.

“Timu yetu ya Serengeti boys, inahitaji gharama nyingi ili kufanikisha safari ya kwenda Gabon katika fainali hizo za vijana, nitoe ombi kwa Watanzania wote kuichangia timu yao kiasi chochote cha fedha kupitia namba (22344) ili kufanikisha safari hiyo," alisema mwenyekiti wa kamati, Charles Hilary.

Aliongeza kuwa michango ya Watanzania ndiyo itafanikisha safari ya timu hiyo ambayo lengo lake ni kufanya vizuri na hatimaye kukata tiketi ya kushiriki fainali za vijana za dunia.

Habari Kubwa