Michuano gofu kufanyika Arusha

09Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Michuano gofu kufanyika Arusha

CHAMA cha Gofu Tanzania (TGU), kimesema kuwa mashindano ya wazi ya mchezo huo yamepangwa kufanyika kuanzia Novemba 29 hadi Desemba Mosi mwaka huu kwenye viwanja vya Kili Golf Wildlife jijini Arusha.

Shindano hili ambalo ni mahsusi kwa wachezaji wa Kundi A wenye "handicap kuanzia 0 hadi 9, limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya TGU na Taasisi ya Verge Africa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa TGU, Chris Martin, alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yako katika hatua za mwisho na chama kinatarajia michuano hiyo kuwa na ushindani zaidi.

Martin alisema kuwa katika wachezaji wa Kundi A wenye "handicap 0 hadi 9 yatashirikishwa pia makundi mengine matatu ambayo ni Kundi B la wachezaji wanaume wenye "handicap 10 hadi 18 na lingine la Wazee "Senior players" wenye umri kuanzia miaka 6.

Alisema kuwa wapo wachezaji watakaoshiriki ambao wana handicap 10 hadi 18 na wachezaji wa kulipwa.

"Kundi A litacheza mashimo 72 kwa siku 3 na makundi mengine yanayoshirikishwa yatacheza katika mashimo 36 tu kwa siku mbili.

Mshindi kwa Kundi A atapatikana kutokana na idadi ya jumla ya mikwaju atakayocheza mchezaji katika mashimo 72. Kwa makundi mengine mshindi atapatikana kwa "Net score" kutokana na mashimo 36," alisema Martin.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hakuna mchezaji atakayeruhusiwa kucheza zaidi ya handicap 18 na usajili wa wachezaji wanaotarajiwa kushiriki ufungwa Novemba 22, mwaka huu.

Aliwataka wachezaji wote wa hapa nchini kujisajili kupitia katika klabu zao huku wale wa kimataifa kuwasiliana na chama ili kufahamu taratibu za kujiandikisha.

Habari Kubwa