Michuano ya Chalenji kuanza Des. 1 Kampala

23Oct 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Michuano ya Chalenji kuanza Des. 1 Kampala

BARAZA la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), limesema kuwa mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Chalenji yamepangwa kufanyika kuanzia Desemba 1 hadi 19 mwaka huu jijini Kampala, Uganda, imefahamika.

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, picha mtandao

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema jana kuwa maandalizi kuelekea mashindano hayo yameshafanyika na kuzitaja nchi zilizothibitisha kushiriki michuano hiyo ni 11.

Musonye alizitaja nchi hizo wanachama kuwa ni pamoja na wenyeji Uganda, Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Kenya (Harambee Stars), Burundi, Somalia, Djibouti, Zanzibar (Zanzibar Heroes), Eritrea, Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia.

"Tunafuraha kusema kuwa Cecafa imepokea maombi kutoka katika nchi tatu ambazo zinataka kushiriki mashindano haya kama wageni na tutayafanyia kazi maombi yao," alisema Musonye.

Kiongozi huyo alisema kuwa ratiba ya mashindano hayo itatolewa ifikapo Novemba Mosi mwaka huu, baada ya kufunga dirisha la nchi wanachama kuthibitisha ushiriki wao.

"Tunawashukuru wanachama wetu ambao wamekubali kuwa wenyeji wa mashindano haya, pamoja na nchi zilizokubali kushiriki kwenye michuano hii mitatu, ambayo itakamilisha kalenda ya matukio kwa mwaka huu," Musonye alisema.

Aliongeza kuwa pia baraza hilo liko katika hatua za mwisho za maandalizi ya mashindano ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 14 hadi 23 mwaka huu hapa jijini Dar es Salaam.

Alizitaja nchi zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika kwa mara ya tatu kuwa ni pamoja na wenyeji Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), Uganda, Burundi, Djibouti, Zanzibar, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini.

"Ratiba ya mashindano haya ya Kombe la Chalenji kwa wanawake inatarajiwa kutolewa kesho (leo), tayari maofisa wa Cecafa walifika Dar es Salaam wiki iliyopita ili kuangalia maandalizi yalipofikia, tunafuraha kusema kuwa, kila kitu kimekwenda vema, TFF iko tayari kuandaa michuano hii," aliongeza kiongozi huyo.

Pia alisema kuwa Uganda itakuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana ya umri chini ya miaka 17, ambayo pia yatachezwa kuanzia Desemba 1 hadi 19 mwaka huu nchini humo.

Habari Kubwa