Michuano ya mabunge kufanyika Desemba Dodoma

03Nov 2017
Renatha Msungu
Nipashe
Michuano ya mabunge kufanyika Desemba Dodoma

MICHUANO ya Jumuiya ya mabunge ya Afrika Mashariki imepangwa kufanyika Desemba Mosi mkoani hapa kwa kushirikisha nchi saba zilizo ukanda huu.

Mwenyekiti wa Bunge Sport, William Ngeleja.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bunge Sport, William Ngeleja wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya michezo hiyo.

Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema, aliitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni pamoja na soka, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa kikapu pamoja na gofu.

Alisema mbali na michezo hiyo pia kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa washiriki wa mashindano hayo.

"Sisi kama Bunge Tanzania tunaendelea na maandalizi ya mashindano haya ambayo tunaamini yataleta msisimuko mkubwa," alisema Ngeleja.

Alisema kuwa kutakuwa na zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa washindi wa mashindano hayo.

Kwa upande wa maandalizi ya timu ya Bunge la Tanzania, Ngeleja, alisema kuwa yanaendelea vizuri.

Alisema timu za nchi jirani zisiwe na wasiwasi kutokana na kile anachoamini kila kitu kiko sawa kwa ajili ya maandalizi.