Minziro apewa mikoba ya Popadic Singida United

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Minziro apewa mikoba ya Popadic Singida United

UONGOZI wa Klabu ya Singida United umetangaza kumsimamisha kazi kocha wa timu hiyo, Dragan Popadic na nafasi yake kuchukuliwa na Fred Felix Minziro.

Mkurugenzi wa timu hiyo, Festo Sanga, aliliambia Nipashe jana kwamba kumekuwa na msuguano kati ya Popadic na wachezaji wa timu hiyo hali iliyosababisha uongozi wa Singida kuamua kumsimamisha kocha huyo.

"Kwa sasa timu tumemkabidhi Minziro 'Baba Isaya', ambaye ataiongoza timu kwa kipindi hiki kilichobaki," alisema Sanga.

Inaelezwa wachezaji wa timu hiyo hawafurahishwi na uongozi wa kocha Popadic ambaye amekuwa mkali na asiyetaka ushauri wa mtu.

Singida United imekuwa kwenye hali mbaya ndani ya uwanja tangu kuondoka kwa kocha Hans van der Pluijm na baadhi ya nyota wake ambao pamoja na Pluijm walijiunga na Azam FC.

Hata hivyo, Pluijm hakukaa na Azam baada ya uongozi wa klabu hiyo kuamua kumtimua pamoja na msaidizi wake Juma Mwambusi kutokana na matokeo mabaya.

Habari Kubwa