Minziro kuipaisha Singida United

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Minziro kuipaisha Singida United

WAKATI zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza, Kocha Mkuu wa Singida United, Felix Minziro, amesema kikosi chake kimefanya maandalizi mazuri na ana uhakika wa kufanya vizuri msimu huu.

Felix Minziro.

Singida United ambao huu utakuwa ni msimu wa tatu kwao kushiririki Ligi Kuu Bara tangu ilipopanda msimu wa 2017/18, msimu uliopita imaliza katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.

Ilishinda mechi 11, ikapoteza 13 na kutoka sare 14 huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu mabao 39 na ile ya ushambuliaji ikifumania nyavu mara 30 tu.

Hata hivyo, Minziro aliyeanza kukinoa kikosi hicho wakati msimu ukielekea ukingoni, amepania kuuanza vema msimu huu, unaotarajiwa kuanza kufurukuta Agosti 23, mwaka huu.

"Wachezaji wanaendelea kupambana na wana kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya msimu ujao.

"Tunatarajia ushindani utakuwa mkubwa nasi pia tumejipanga kufanya vizuri kikubwa tunahitaji sapoti kutoka kwa mashabiki na wadau wote," alisema Minziro ambaye amekuwa akiziokoa timu nyingi za Ligi Kuu zinazochungulia kushuka daraja, huku pia akiwa na rekodi nzuri ya kupandishi timu Ligi Kuu Bara.