Mkopi Mchezaji Bora Februari

10Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar
Nipashe
Mkopi Mchezaji Bora Februari
  • Straika huyo wa Tanzania Prisons tayari ametupia mabao sita msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

MSHAMBULIAJI wa Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Februari kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mshambulaiji wa Prisons ya Mbeya, Mohamed Mkopi akimtoka beki wa JKT Ruvu, George Minja.

Katika mechi nne za mwezi uliopita, Mkopi alianza kwenye kikosi cha 'Wajelajela' kilichotoka sare dhidi ya Yanga (2-2), Mbeya City FC (0-0), Mwadui (1-1) na Mgambo Shooting (1-1) akitoa mchango mkubwa kwa akifunga bao moja na kupika mawili.

Mshambuliaji huyo ambaye kabla ya mechi yao ya jana dhidi ya Kagera Sugar alikuwa amefunga mabao sita kwenye ligi hiyo, aling'ara zaidi katika mechi mbili kati ya nne alizopangwa kwenye kikosi cha Salum Mayanga mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkopi alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi walipocheza dhidi ya Mwadui mkoani Shinyanga na ile dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kwa kunyakua tuzo hiyo straika huyo atazawadiwa shilingi milioni moja na wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya huduma za mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Mkopi anaaungana na kiungo Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba 2015) na beki Shomari Kapombe wa Azam FC (Januari 2016) kutwaa tuzo hiyo msimu huu.

Habari Kubwa