Mkude aeleza namna Simba itakavyoshinda

15Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Mkude aeleza namna Simba itakavyoshinda

WAKATI ikiwa imebaki siku moja kabla ya mchezo wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuchezwa, kiungo wa Simba, Jonas Mkude, amesema anaamini wachezaji wenzake watakaopangwa katika mechi hiyo watapambana na kuhakikisha "wanakisambaratisha" kikosi cha AS Vita.

Simba inatarajia kuwakaribisha AS Vita katika mechi yake ya mwisho ya Kundi D itakayochezwa kesho kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mkude, nahodha wa zamani wa Simba hatacheza mechi hiyo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkude alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekuwa bora zaidi kuliko walivyofanya katika mechi nyingine kwa sababu wanahitaji ushindi na si matokeo mengine.

"Nitaukosa mchezo wa Jumamosi, lakini Simba ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, nina imani wachezaji wenzangu watapambana kwa ajili ya timu ili ipate ushindi, kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo huu ambao tunaucheza kwenye uwanja wa nyumbani," alisema Mkude.

Aliongeza kuwa ndoto ya wachezaji wote wa Simba ni kuona wanatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na wanafahamu wanachohitaji ni matokeo ya ushindi pekee.

“Kikubwa ninachoweza kusema ni mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani, tupo nyumbani na wao wanajua umuhimu mkubwa sana kwetu kuweza kufanya vizuri," alisema kiungo huyo ambaye alipandishwa akitokea katika timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (Simba B).

Tayari kikosi cha AS Vita kimeshawasili nchini kwa ajili ya mchezo huo ambao utatanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Al Ahly dhidi ya JS Saoura itakayochezwa Misri.

Mara ya mwisho Simba kutinga hatua ya robo fainali ilikuwa ni mwaka 2003, wakati klabu hiyo ilikaa miaka 15 ili kucheza tena hatua ya makundi.