Mkude awangukia mashabiki Simba kipigo Lyon

08Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkude awangukia mashabiki Simba kipigo Lyon

NAHODHA wa Simba, Jonas Mkude amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kufuatia kipigo cha bao1-0 walichokipata juzi kutoka kwa African Lyon.

Mkude aliliambia Nipashe jana kuwa, wamepoteza mchezo huo kutokana na makosa ya uwanjani lakini bado wana nia na kiu ya kutwaa ubingwa msimu huu.

"Tunafahamu mashabiki wameumia kwa matokeo ya jana ambayo hawakuyategemea, tunawaomba radhi na tuendelee kushikamana kuelekea kwenye mchezo unaofuata," alisema Mkude.

Alisema mchezo wa juzi walikuwa na nia ya kushinda, lakini mambo hayakuwa mazuri kwao.

"Mchezo ulikuwa mgumu kwa sababu wapinzani wetu walikuwa 'wakipaki basi' muda wote wa mchezo na wametumia vizuri nafasi
waliyoipata,"alisema Mkude.

Alisema kwa sasa wanaelekeza akili zao kwenye mchezo wa kesho watakaocheza ugenini mkoani Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons.
Pamoja na kupoteza mchezo wa juzi, Simba wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 35 wakifuatiwa na Yanga yenye pointi 30 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo14.

Toto African ya Mwanza inaburuza mkia ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo 15.

Habari Kubwa