Mkutano Mkuu TFF leo

12Mar 2016
Somoe Ng'itu
Tanga
Nipashe
Mkutano Mkuu TFF leo

MKUU wa Mkoa Tanga, Mwantumu Mahiza anatarajiwa kufungua mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika leo jijini hapa.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika.

Alisema kuwa wajumbe wa mkutano huo walipewa agenda katika muda unaotakiwa kama katiba ya shirikisho inavyoelekeza.

“Maandalizi ya mkutano yamekamilika, zaidi ya nusu ya wajumbe wameshawasili,” alisema Mwesigwa.
Mwesigwa alisema mkutano huo utakuwa na agenda 13 na miongoni mwao, ipo agenda ya marekebisho ya katiba ya TFF kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwakani.

Kipengele kinachotajwa zaidi katika mabadiliko hayo ni kupunguza idadi ya wapigakura na kuruhusu mwenyekiti tu kubeba dhamana hiyo.

“Kama badiliko hili litapita, litakuwa na madhara makubwa. Tunachotaka kwa sasa ni kuhakikisha kipengele hiki hakifanyiwi marekebisho,” alisema mjumbe mmoja kutoka Dodoma bila kutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti.

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kumalizika kesho kwa wajumbe kuweka jiwe la msingi kwenye uwanja wa michezo unaojengwa na TFF.

Habari Kubwa