Mkwabi afunguka sintofahamu Simba

06Jul 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mkwabi afunguka sintofahamu Simba
  • ***Ashangazwa kuhusika kuhujumu klabu hiyo pamoja na mgawanyiko uliopo...

WAKATI wingu na hofu limeendelea kutanda ndani ya Simba kufuatia sintofahamu iliyopo kati ya viongozi na mwekezaji wa klabu hiyo, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji "MO",-

Swedi Mkwabi.

kiongozi mkuu wa mabingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Swedi Mkwabi, ameibuka na kusema naye anashangazwa na hali hiyo iliyopo.

Hofu ya "ndoa" kati ya MO na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kutaka kuvunjika ilianza kuzungumzwa zaidi ya miezi miwili na taarifa za ndani zinaeleza kuwa hali hiyo imekuja kutokana na kuwapo kwa tofauti kati ya viongozi na mwekezaji huyo wa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya MO kuanza kuandika mfululizo wa ujumbe mbalimbali zenye "mafumbo" katika kurasa zake za kijamii na kuzidisha mijadala miongozi mwa wanachama, mashabiki wa Simba na wadau mbalimbali wa soka hapa nchini.

"Kwenye uongozi, na kwenye maisha, huwa nakaribisha kukosolewa. Lakini siwezi na sikubali kufanya kazi na mtu anayejuhumu malengo, mipango na maslahi mapana ya taasisi, mtu anayetoboa mtumbwi tunaosafiri nao," MO aliandika ujumbe huo katika ukurasa wake huku akiweka picha inayomwonyesha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (kushoto) na kulia ni Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkwabi, alisema kuwa hata yeye binafsi haelewi sintofahamu hiyo iliyopo ndani ya klabu yao ambayo kwa sasa iko kwenye mchakato muhimu wa kukamilisha usajili kwa lengo la kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.

Mkwabi alisema kuwa kama kiongozi mkuu, hafurahishwi na hali hiyo kwa sababu haileti "afya" ya maendeleo ya klabu yao na mpira wa miguu hapa nchini.

Hata hivyo, Mkwabi alisema kwamba anasikitishwa zaidi kuona yeye akihusishwa katika sintofahamu hiyo, bila ya kufahamu sababu za msingi.

"Hata sielewi, hata mimi ninashaa, ninatajwa kuhusika kushirikiana na ( majina tunayahifadhi) ili kuzuia mambo yao," alisema kwa kifupi kiongozi huyo ambaye aliingia madarakani katika uchaguzi wa klabu hiyo uliofanyika Novemba mwaka jana chini ya katiba mpya ambayo imempa nguvu mwekezaji asilimia 49 na asilimia 51 zimebakiwa kwa wanachama.

Taarifa za ndani za klabu hiyo zinasema kuwa moja ya sababu ambazo zimepelekea pande hizo mbili kutofautiana, ni kutofanya uamuzi wa pamoja wa mambo mbalimbali yanayoihusu timu yao, ikiwamo suala la usajili wa wachezaji wapya na wale wa zamani, wanaopewa mkataba mipya.

Imeelezwa kuwa, mchakato wa usajili unaendelea klabuni hapo, umesaidia kuwatuliza wanachama ambao wanaamini ujio wa mwekezaji huyo, ulichangia kwa kiasi kikubwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika.