Mkwasa akabidhi ripoti ya usajili

28Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mkwasa akabidhi ripoti ya usajili

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa, amesema tayari amekabidhi ripoti kwa uongozi wa timu hiyo na kuonyesha nafasi sita za usajili ikiwemo golikipa ili kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Mkwasa alisema uongozi umeshaanza kufanyia kazi ripoti yake ikiwamo kutafuta mbadala wa Edward Manyama ambaye ameondoka ndani ya kikosi cha timu hiyo na kusajili na Azam FC.

"Msimu huu hatukufikia malengo yetu kutokana na kuandamwa na majeruhi, sasa nimeeleza uongozi wangu kupitia ripoti yangu kusajili wachezaji ambao wataleta ushindani na kuwepo kwa kikosi kipana na kufikia malengo yetu kwa msimu ujao," alisema Mkwasa.

Alisema umakini katika usajili unatakiwa kulingana na mipango yao ya msimu ujao kutaka kuleta ushindani mkubwa katika ligi hiyo ambayo hutarajia kuanza muda sio mrefu.

"Hatuna muda tunatakiwa kufanya kila kitu mapema, kusajili wachezaji wazuri pamoja na kuanza mapema maandalizi ya msimu, usajili utakapokamilika tunatarajia kuanza maandalizi ya msimu," alisema Mkwasa.