Mkwasa aupotezea ubingwa wa Ligi Kuu

23Nov 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mkwasa aupotezea ubingwa wa Ligi Kuu

​​​​​​​LICHA ya timu yake kuendelea kuwa na matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa, amesema hafikirii kukipa nafasi kikosi chake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga amesema malengo yao ni kuona wanamaliza msimu huu kwenye nafasi tano za juu.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mkwasa alisema wamefanya maandalizi ya kupambana na ushindani na vile vile kutafuta matokeo mazuri katika kila mechi ili kumaliza kwenye nafasi nzuri.

Alisema mikakati yao ni kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri katika mechi hizo na ikatokea akapoteza ana imani ni suala la mpira ambalo lipo.

"Kwa sasa tunafikiria kutafuta matokeo katika mechi ili kumaliza ligi bila ya presha, kwa msimu huu hatuna wazo la ubingwa sababu ya maandalizi tuliyoyafanya mwanzoni mwa msimu huu, kwa ajili ya kutafuta matokeo ambayo tutaendelea kubaki katika ligi pamoja na kuandaa vijana," alisema Mkwasa.

Aliongeza uamuzi wa kuwaamini wachezaji vijana umeisaidia kufanya vyema na ataendelea kuwapa nafasi kwa sababu timu hiyo inasimamiwa na taasisi ambayo haina uwezo wa kusajili nyota wa kulipwa ambao wanahitaji kulipwa gharama kubwa.

"Kuwaamini vijana katika timu yangu na kunipa matokeo mazuri ni jambo la kujivunia, hii sio kwa ajili ya Ruvu pekee pia watakuja kutusaidia hapo baadaye katika timu zetu za Taifa watakapoonekana na kuaminika," alisema Mkwasa.

Aliongeza kikosi chake kinaendelea kuimarika na vijana hao kumpa matokeo mazuri ikiwamo ushindi wa juzi dhidi ya Mbeya City, nyota wake wanazidi kuimarika na wanajiamini kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mechi zinazofuata.

Ruvu Shooting juzi ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City na kupaa hadi kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 19.

Habari Kubwa