Mngazija, Is-haka wang'ara Zanzibar

15Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Mngazija, Is-haka wang'ara Zanzibar

KAMATI ya mashindano ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) imetangaza Kocha wa Selem View inayoshiriki Ligi Kuu Visiwani hapa, Ali bakari Mngazija kuwa Kocha Bora wa Februari.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Hussein Ahmada alisema kuwa Mngazija alipata kura 40 huku mpinzani wake ambaye ni Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msimu, amepata kura 35.

Ahmada alisema kuwa ili kumpata mshindi wa tuzo hiyo, kura zilipigwa kupitia mitandao ya kijamii inayoendeshwa na chama hicho ya akaunti za Twitter, Instagram pamoja na facebook kwa kuwapa wadau wake fursa ya kuteua mshindi.

Ahmada aliongeza kuwa katika kuchagua mshindi wa tuzo hiyo, makocha watashindanishwa kwa kuangalia vigezo mbalimbali ikiwamo kuangalia matokeo ya uwanjani katika mechi za mzunguko wa pili ambazo zimeanza hivi karibuni.

Mngazija amepewa zawadi ya cheti pamoja na Mchezaji Bora wa mwezi uliopita, Is-haka Omar ambaye pia anatokea Selem View baada ya kupata kura 30 dhidi ya Abdul Yusuph wa KVZ ambaye alipata kura 17.

Kiongozi huyo wa ZFA amewaomba wadau kujitokeza ili kufadhili tuzo hizo kwa ajili ya kuongeza hamasa kwa makocha na wachezaji wanaoshiriki ligi hiyo kujituma zaidi.

Habari Kubwa