Mnyate:Hazard wa Bongo aliyeipa Yanga ubingwa

11May 2016
Adam Fungamwango
Lete Raha
Mnyate:Hazard wa Bongo aliyeipa Yanga ubingwa

EDEN Hazard wa Chelsea alifunga bao dakika ya 83 lililoifanya timu yake kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Tottenham wikiendi iliyopita.

Jamal Mnyate (kushoto)

Ni goli ambalo liliipa ubingwa wa England, Leicester City ambayo haikuwa na mechi yoyote siku hiyo.

Maili nyingi kutoka huko, nchini Tanzania mchezaji wa Mwadui FC, Jamal Mnyate anafanya kama alivyofanya Hazard.
Ilikuwa ni Mei 8, wakati mchezaji huyo wa zamani wa Azam na Mtibwa Sugar alipofunga bao katika dakika ya 73, na kuifanya timu yake ya Mwadui FC kushinda bao 1-0 dhidi ya Simba.

Kama ilivyokuwa na Chelsea, bao la Hazard halikuinufaisha timu yake tu, bali pia kuipa ubingwa Leicester City, bao la Mnyate pia hakuinufaisha Mwadui tu. Liliipa ubingwa wa Tanzania Bara Yanga iliyokuwa nayo haina mechi yoyote siku hiyo.

Kama ambavyo Leicester City ilipochukua ubingwa ikiwa na pointi nyingi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ikiwa imebakisha mechi tatu, Yanga pia ilitwaa ubingwa ikiwa nayo imebakiwa na mechi tatu, huku pointi zake zikiwa haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Ndiyo maana mara baada ya mechi hiyo, Mnyate amepachikwa jina na kuitwa Hazard wa Bongo kutokana na mfanano huo.

Mchezaji huyo anayecheza wingi ya kushoto 'aliwakomba' mabeki wa Simba mmoja baada ya mwingine na kuingia ndani ya eneo la hatari, mwili wake na mguu ukiwa umeelekea upande wa kulia.

Ghafla aligeuka na kuachia shuti dhaifu, lakini la akili upande wa kushoto mwa golikipa Vincent Angban, ambaye hakujisumbua hata kutingishika.

Cha ajabu ni kwamba Simba ilipata nafasi kadhaa kama hizo, ikiwa na wachezaji wa kimataifa, lakini hawakuweza kufanya kama Mnyate.

Kwa baadhi ya mashabiki wanaolifuatilia soka kijuujuu, linaweza kuwa ni jina geni kwenye medani ya soka nchini.

Hata hivyo, wale wanaolifuatilia kwa ndani, jina hili si geni kwani ni mmoja wa wachezaji wa kwanza kabisa kuichezea Azam FC msimu wa kwanza baada ya kupanda Ligi Kuu 2008/09.

Rekodi zinaonyesha kuwa si mara ya kwanza kuifunga Simba, kwani msimu huo wa kwanza Azam ilipoifunga Simba mabao 2-0 Oktoba 4, 2008, Mnyate alifunga goli la kwanza, huku la pili likiwekwa na mchezaji wa zamani wa Wekundu hao, Shekhan Rashid.

Msimu wa 2011, Azam ilimtoa kwa mkopo kwenda Moro United kwenye kipindi cha dirisha dogo.

Baadaye alijiunga na Mtibwa Sugar, timu aliyoichezea hadi 2015 mkataba wake ulipomalizika na kujiunga na Mwadui FC.

Alizaliwa Septemba 22, 1992 na ana uzito wa kilo 65 kwa sasa.

Winga wa zamani wa Simba Ulimboka Mwakingwe anasema kuwa aliwapa ushauri viongozi na na benchi la Simba kuwasajili wachezaji Atupele Green ambaye kwa sasa yupo Ndanda FC akiwa tayari ameshafunga magoli 11, Mudhamir Yassin ambaye yuko Mtibwa na Mnyate, lakini wakampuuza na madhara yake ndiyo haya yanayoonekana sasa.

Habari Kubwa