Mo akata mzizi wa fitina Djuma Simba

20Sep 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mo akata mzizi wa fitina Djuma Simba
  • ***Aussems ashinda vita baada ya uamuzi kutolewa, kuivaa Mbao FC akiwa...

WAKATI siku za kocha msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, kukaa katika klabu hiyo zikiwa zimemalizika baada ya mwekezaji, Mohammed "Mo" Dewji kutoa uamuzi wake,-

Mohammed "Mo" Dewji.

Kikosi cha mabingwa hao kinatarajia kuwavaa Mbao FC leo katika mechi ya raundi ya nne ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kikiwa na ari ya ushindi.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinaeleza kuwa Mo ameamua kusikiliza uamuzi uliofikiwa na Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems, ambaye hataki kuendelea kufanya kazi na Mrundi huyo.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa kuchelewa kutimuliwa kwa Djuma kunatokana na busara za viongozi waliopo, lakini baada ya Mo kufanya mazungumzo na Aussems ndiyo kumemaliza hatima ya mrundi ndani ya Simba.

"Sisi ndio kama tulikuwa tunapambana kujaribu kuyaweka haya mambo sawa, lakini imeshindikana, unajua mzungu hawezi kuishi kinafiki kama sisi, ila alijaribu kumvumilia na sasa ikafikia wakati ameona hawezi kulazimisha kufanya naye kazi," alisema kiongozi mmoja wa juu wa Simba.

Kiongozi huyo alisema pia suala la kudaiwa kutokuwa na nidhamu lilikuwa ni moja ya kosa ambalo limeonekana kumkera Aussems katika kipindi chote ambacho amekuwa akifanya kazi na Djuma.

Hata hivyo, viongozi wa Simba wamekuwa kimya na kukataa kuweka wazi hali ya kutokuelewana kwa makocha hao hata pale Djuma alipoachwa kwenye msafara wa timu hiyo wakati ikienda Mtwara kuwakabili Ndanda FC na juzi ilipoelekea Mwanza kuwavaa Mbao FC.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kikosi cha wachezaji 20 kilifika salama Mwanza na jana jioni walitarajia kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ya leo.

Simba itashuka uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kufungana na Ndanda FC, lakini ikiwa na pointi saba sawa na Mbao FC inayofundishwa na beki wa zamani 'Wekundu wa Msimbazi' hao, Amri Said.

Habari Kubwa