MO awageukia wachezaji Simba

05Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
MO awageukia wachezaji Simba
  • *** Awataka kutambua thamani ya kuvaa jezi ya klabu hiyo na kuahidi…

MSHINDI wa zabuni ya ununuzi wa hisa za Klabu ya Simba, Mohamed "MO" Dewji , amewataka wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa kujituma na kutambua thamani ya kuvaa jezi ya klabu hiyo.

Dewji, alisema Simba ni klabu kubwa na wachezaji wanaopata nafasi ya kuichezea wanapaswa kujituma na kuonyesha uwezo unaoendana na jina la klabu hiyo.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Dewji, alisema kuwa kama wachezaji watapambana uwanjani na kujituma, wananafasi kubwa ya kuiletea timu hiyo mafanikio.

“Simba ni timu kubwa, nimekuwa shabiki wa timu hii tangu nikiwa mtoto, nilipanga kwa miaka mingi lazima nije kuisadia timu hii, wachezaji wetu wanapaswa kutambua thamani ya kuvaa jezi ya timu hii, ni lazima wajitume uwanjani ili kuipa mafanikio,” alisema Dewji.

Aidha, alisema atakuwa karibu na wachezaji kuhakikisha wanaitumikia klabu hiyo katika mazingira mazuri yatakayowafanya kujituma uwanjani.

“Mambo yakishakamilika (taratibu za kubadili mfumo wa uwendeshwaji), Simba haitakuwa timu ya kuwania ubingwa wa ndani pekee, itakuwa timu ya kuwania ubingwa wa Afrika na kushindana na timu nyingine kubwa Afrika,” aliongeza kusema.

Jumapili iliyopita Dewji ambaye ni mfanyabiashara maarufu na mwanachama wa klabu ya Simba ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, alitangazwa na aliyekuwa Mwenyejiki wa Kamati ya Zabuni ya klabu hiyo kuwa ndio mshindi wa zabuni ya kununua hisa asilimia 50 za klabu hiyo.

Dewji atawekeza kiasi cha Sh. bilioni 20 kwa ajili ya kununua hisa asilimia 50 na kubadili uwendeshwaji wa klabu hiyo ambayo itajiendesha kwa mfumo wa kampuni.