Mo Salah: Nipo tayari kustaafu

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mo Salah: Nipo tayari kustaafu
  • ***Kama ukiniuliza mimi kuhusu mikataba, nitapenda kubaki hapa hadi siku ninastaafu, lakini siwezi kulizungumzia sana...

WAKATI ulimwengu wa soka ukiendelea kufuatilia ni nini kitatokea kwa Mohamed Salah wakati mkataba wake unaelekea ukingoni, yeye mwenyewe amesafisha hali ya hewa kuhusu majaliwa yake.

Akizungumza kabla ya mchezo wa jana Jumapili ambao Liverpool ilikuwa ikicheza na wapinzani wao wakuu kwenye Ligi Kuu England, Manchester United, Salah alionyesha nia ya kutaka kubakia kwenye dimba hilo la Anfield.

Salah amesema kwamba, malengo yake ni kumalizia soka lake hapo Liverpool, lakini yeye si mwamuzi wa mwisho kuhusu hilo.

“Kama ukiniuliza mimi (kuhusu mikataba), nitapenda kubaki Liverpool hadi siku ninastaafu soka, lakini siwezi kulizungumzia sana hilo, halipo mikononi mwangu,” alisema Salah akinukuliwa na Sky Sport.

“Inategemea na klabu inataka nini, si (mimi) ninataka nini. Kwa sasa, sijioni nikicheza dhidi ya Liverpool, lakini tutaona nini kitatokea baadaye.”

Kwa siku za karibuni, Liverpool wamemalizana na habari za mikataba mipya kwa baadhi ya wachezaji muhimu kwenye kikosi chao.

Kinachofikirisha ni mkataba wa Salah ambaye amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake lakini, hadi sasa hakijaeleweka.

Mapema hivi karibuni ESPN ilimnukuu wakala wake akisema kwamba, Salah anataka kuongezewa mshahara hadi pauni 400,000 kwa wiki ili aweze kukubali kusaini mkataba mpya na 'Wekundu' hao.

Hadi sasa Salah ameshapachika mabao 12 katika michezo 11 aliyoitumikia Liverpool msimu huu kwenye michuano yote, kabla ya mechi ya jana Jumapili dhidi ya Man City.

Habari Kubwa