Moris hatihati kuikosa Afcon

17Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Moris hatihati kuikosa Afcon

HALI ya beki wa kati wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Aggrey Moris, kuweza kuitumikia timu yake katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, ambazo zitaanza Ijumaa nchini Misri, iko mashakani, imefahamika.

Taifa Stars inayofundishwa na Mnigeria Emmanuel Amunike, itaanza kutupa karata yake ya kwanza katika fainali hizo Jumapili dhidi ya wenzao wa Senegal.

Moris, beki mkongwe wa mabingwa wa Kombe la FA Tanzania, Azam FC aliumia mguu katika mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji Misri, na jana hakuwa sehemu ya kikosi kilichoshuka dimbani kuivaa Zimbabwe.

Akizungumza na Nipashe kutoka jijini Cairo jana, Meneja wa Stars, Danny Msangi, alisema tayari beki huyo ameshafanyiwa vipimo vya MRI na hatima yake kuelekea mashindano hayo ilitarajiwa kujulikana jana jioni.

Msangi alisema kwa sasa kocha Amunike anaendelea na maandalizi yake kwa sababu anafahamu kila nafasi ina wachezaji zaidi ya mmoja.

"Ni mgonjwa na ameshafanyiwa vipimo, leo (jana) jioni ndio tutajua nini nafasi yake," Msangi alisema kwa kifupi.

Amunike alitarajiwa kutumia wachezaji tofauti na wale walioivaa Misri, katika mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe uliotarajiwa kufanyika jana usiku.

Habari Kubwa