Morocco: Yanga imepita, tunageukia Wasudan CAF

24Nov 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Morocco: Yanga imepita, tunageukia Wasudan CAF

BAADA ya kuanza mechi yake ya kwanza kwa sare ya bao 1-1, Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemed Morocco, amesema kwa sasa wanasahau matokeo hayo dhidi ya Yanga, na kuelekeza akili na nguvu zao kwenye michuano ya kimataifa, wakati huu wakitarajia kuikaribisha ...

Ali-Rabita FC ya Sudan Kusini katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Morocco ambaye amerithi mikoba ya Thierry Hitimana aliyetimuliwa wiki iliyopita kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo, Jumamosi ataiongoza Namungo katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa katika Uwanja wa Azam Complex kabla ya timu hizo kurudiana nchini Sudan Kusini kati ya Desemba 4-6, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Morocco alisema mechi dhidi ya Yanga ilikuwa kipimo tosha kwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo huku akifafanua kuwa, licha ya kutopata nafasi ya kuwaona wapinzani wao, ana imani na uzoefu alionao katika michuano ya kimataifa atapambana ili kufanya vizuri kulingana na kikosi alichokuwa nacho.

Alisema kikubwa ambacho anakifanya ni kuangalia wachezaji ambao alionao kwa sasa pamoja na aina ya mazoezi atakayowapa kuelekea mechi hiyo.

“Sina presha juu ya michuano hiyo, licha ya kutopata nafasi ya kuwaona wapinzani wetu, nina uzoefu mkubwa wa michuano ya CAF, kilichobaki kwa sasa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wangu ili kuachana na matokeo ya Yanga na kuelekeza akili kwenye michuano hiyo,” alisema Morocco.

Alisema tatizo la Namungo aliloliona kabla ya kukutana na Yanga, wakati akifuatilia Ligi Kuu Bara lilikuwa ni umaliziaji kwenye safu ya ushambuliaji, hivyo atalifanyia kazi.

“Kuna makosa madogo madogo kwa mabeki ikiwamo kutokuwa makini katika mipira ya faulo pamoja na kona, hilo limetugharimu kwa mechi yetu hii dhidi ya Yanga kwa kuruhusu bao kabla ya kujipanga na hatujasawazisha,” alisema Morocco.

Alisema anapenda aina ya makipa ambao wanatoka na kwenda kuongeza mashambulizi hali ambayo amekuwa akiifanya kipa wao, Jonathan Nahimana, baada ya kutoka mita 30 ndani ya eneo lake katika mechi dhidi ya Yanga.

“Huwa napenda aina ya kipa kama huyu, tutambue naye ni mchezaji hiyo katika mpira wa kisasa naye anatakiwa kwenda kufanya mashambulizi na kuwa makini hasa tunapokuwa tukishambulia,” alisema.

Kwa matokeo hayo ya jana, Namungo inaendelea kushika nafasi ya tisa kwenye msmamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 15 wakati Yanga ambayo imefikisha alama 25 sawa Azam FC iliyopo kileleni, imeshindwa kuwashusha 'Wanalambalamba' hao kutokana na kuwa na tofauti nzuri zaidi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Habari Kubwa