Morrison ajikaanga, mguu ndani, nje

14Jul 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Morrison ajikaanga, mguu ndani, nje

KITENDO cha mchezaji wa kimataifa wa Yanga, winga Mghana Bernard Morrison, kufanyiwa mabadiliko katika mechi dhidi ya Simba juzi na kuamua kutoka moja kwa moja uwanjani badala ya kukaa kwenye benchi na wenzake, kimeukera uongozi wa Yanga na kuahidi kujifungia kumjadili kabla ya kutoa uamuzi mzito .

Winga wa Yanga, Mghana Bernard Morrison, kabla ya mchezo kumkataa na kutolewa uwanjani, akipambana na kiungo mshambuliaji wa Simba raia wa Msumbiji, Luis Miqussone kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA iliyopigwa Uwanja wa Taifa juzi. Simba ilishinda 4-1. MPIGAPICHA WETU

Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la FA iliyopigwa Uwanja wa Taifa juzi na Simba kushinda 4-1, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael alimtoa Morrison dakika ya 79 na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Sibomana, lakini winga huyo hakukaa katika benchi na kuamua kutoka moja kwa moja uwanjani.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mshindo Msolla alisema mchezaji huyo ameonyesha utovu mkubwa wa nidhamu, kitendo ambacho hakijawapendeza wadau wa soka na kuahidi kulitolea maamuzi haraka iwezekanavyo.

“Morrison ameonyesha utovu wa nidhamu kwa kitendo cha kutolewa na kocha na kuamua kutoka nje ya uwanja badala ya kukaa na wachezaji wenzake kwenye benchi, tutakaa sisi kama viongozi tutajua nini tunatakiwa kukifanya,” alisema Msolla.

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Boniface Mkwasa alisema hajafurahishwa na kitendo alichokifanya mchezaji huyo na kuwataka wachezaji wengine kuwa makini pindi wanapokuwa uwanjani ili kujiepusha na masuala kama hayo ambayo hayana afya kwao.

“Morrison amefanya kitendo ambacho hakistahili kufanywa na mchezaji kama yeye ambaye anaangaliwa na wadau wengi wa soka, ilimpasa kubaki na wachezaji wenzake kwenye benchi si kujichukulia maamuzi ya kutoka nje ya uwanja,” alisema Mkwasa, huku Kocha Mkuu, Luc Eymael akikataa kata kata kuzungumzia suala hilo, Nipashe lilipomtaka kutoa maoni yake.

Habari Kubwa