Morrison, Lawi rasmi kifungoni

30Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Morrison, Lawi rasmi kifungoni

​​​​​​​KIUNGO mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Bernard Morrison, amefungiwa kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara na kutakiwa kulipa faini ya Sh. 500,000 kutokana na kumpiga ngumi beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso.

Bernard Morrison.

Morrison alitenda kosa hilo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa mapema wiki hii, ambayo ilimalizika kwa Simba kulala bao 1-0.

Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Nchini (TPLB), imesema adhabu hiyo imetolewa kupitia kanuni ya 39 (5) ya Ligi Kuu inayokataza mchezaji kufanya kosa la kupiga.

Kwa adhabu hiyo, Morrison sasa atakosa mechi dhidi ya Mwadui FC itakayofanyika kesho, Kagera Sugar iliyopangwa kuchezwa Novemba 4, mwaka huu na dhidi ya watani zao Yanga inayotarajiwa kufanyika Novemba 7, mwaka huu.

Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Ghana alionekana akimpiga ngumi Nyosso wakati wachezaji wa Ruvu Shooting wakigomea penalti iliyotolewa kwa wapinzani wao Simba katika mchezo huo.

Wakati huo huo, Gwambina FC imepigwa faini ya Sh. milioni tatu kwa kosa la kuvaa jezi ambazo hazina nembo ya mdhamini katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Pia mchezaji wa Polisi Tanzania, Daruwesh Saliboko, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Gwambina katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Tanzania Prisons yenyewe imetozwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kuingiza magari ya viongozi na mashabiki wakati mchezo kati yake na Simba ukiwa unaendelea huku adhabu ya faini kama hiyo ikimkuta mchezaji wake, Salum Kimenya na kufungiwa miezi mitatu kwa kumpiga ngumi Morrison.

Pia bodi hiyo imemfungia mwamuzi, Shomary Lawi kuchezesha soka kwa mwaka mmoja kwa kushindwa kumudu mchezo huo uliochezwa Oktoba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Habari Kubwa