Morrison: Mengi mazuri yanakuja

24Mar 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Morrison: Mengi mazuri yanakuja

MSHAMBULIAJI wa Yanga ambaye kwa sasa ameiteka mioyo ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, Bernard Morrison, amesema anafurahi kuona 'amekubalika' mapema ndani ya klabu hiyo na hali hiyo inampa nguvu ya kujipanga kufanya makubwa zaidi.

Morrison alisema ili kufikia malengo ya timu hiyo, wachezaji wanahitaji kupambana kuhakikisha wanashinda mechi zao za ligi zilizobakia na mashindano ya Kombe la FA.

Mshambuliaji huyo alisema kuwa 'mapenzi' wanayopata wachezaji wa timu hiyo kutoka kwa mashabiki wa Yanga ni sababu inayowafanya wajitume katika kila mechi wanayocheza na kusahau changamoto zinazowakabili.

"Ningependa kuwashukuru mashabiki kwa kunikubali, nimekuwa na wakati mzuri, nimekuwa nikipata zawadi mbalimbali kutokana na uchezaji wangu, hii inanifanya nijipange zaidi kuisaidia timu yangu, nimejifunza vitu vingi nilipokuwa Orlando Pirates," alisema Morrison.

Hata hivyo alisema ili kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, wanatakiwa kufunga mabao zaidi na hatimaye kujihakikishia nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa na kuwapa furaha mashabiki wao.

"Ninaheshimu ajira yangu ndani ya Yanga, nitaitumikia kwa nidhamu, mipango yangu ni kutimiza malengo yangu, lakini huu ni mpira, kwa sasa naomba nieleweke nguvu na akili zangu nazielekeza kuisaidia Yanga na si timu nyingine," Morrison aliongeza.

Ili kuhakikisha inaendelea kummiliki Mghana huyo, Yanga imempa mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamalizika Juni, 2022 na uamuzi huo ulimaliza tetesi za kujiunga na Simba.

Mshambuliaji huyo aliifungia Yanga bao pekee katika mechi dhidi ya watani zao Simba, ushindi ambao unaendelea kuwapa faraja wanachama wa klabu hiyo ambao baadhi wamekata tamaa ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Habari Kubwa