Mourinho amtupia ‘zigo’ LVG
LONDON, England

22Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mourinho amtupia ‘zigo’ LVG
LONDON, England

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amedai kuwa mwanzo mbaya wa timu yake msimu huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na zama za utawala wa kocha aliyetimuliwa, Louis van Gaal,

kwa mujibu wa vyombo vya habari England.
Mourinho, aliyerithi mikoba ya Van Gaal, yuko kwenye wakati mgumu hivi sasa akishuhudia kikosi chake kikipoteza mechi tatu mfululizo katika mashindano yote.


Sasa anawataka wachezaji wake kujifikiria, kujiamini na kuachana na miaka miwili ya zama za Van Gaal.
Mourinho anaamini kuwa kocha huyo raia wa Uholanzi alitengeneza mfumo ulioruhusu timu kupingwa kila wakati.
Kwa mfano, Mourinho hupenda mabeki wake wa pembeni kupanda mbele kuongeza mshambulizi, mfumo ambao hakuwa akiupa kipaumbele Van Gaal.


Akizungumza Agosti mwaka huu, Mourinho alisema: "Timu yangu ni tofauti na Mr. Van Gaal, ni vigumu kuibaidilisha hali ndani ya muda mfupi.

Ni rahisi kwangu kuwa na wachezaji 20 wapya na kuanza upya kufundisha kuliko kuwa na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa pamoja miaka miwili chini ya kocha mwingine.

"
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea, alijikuta katikati ya lawama Jumapili iliyopita baada ya Man United kufungwa mabao 3-1 na Watford katika mechi ya Ligi Kuu England.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Telegraph, wachezaji wa klabu hiyo wameshtushwa na kauli ya Mourinho.


Hata hivyo, uongozi wa klabu bado una imani na kocha huyo raia wa Ureno.
Kuna taarifa zingine zinadai kuwa nahodha aliye kwenye wakati mgumu, Wayne Rooney anaweza kukaa benchi kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya mabingwa, Leicester City Jumamosi wiki hii.

Habari Kubwa