Mourinho azidi kujitengenezea njia Man U

13Feb 2016
LONDON, England
Nipashe
Mourinho azidi kujitengenezea njia Man U

DANADANA za kocha asiye na kazi kwa sasa, Jose Mourinho kutua ama kutotua Old Trafford zinaendelea na safari hii, kocha huyo Mreno amesema nafasi ya yeye kufundisha Manchester United iko wazi kama timu hiyo itashindwa kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa muda mrefu Mourinho amekuwa akihusishwa kujiunga na klabu hiyo tangu alipotimuliwa Chelsea Desemba mwaka jana.

Kocha wa sasa Man United, Louis van Gaal amekuwa akisisitiza wakati wote kuwa hajaambiwa kama atatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mourinho.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa Mourinho mjini London alidai kuwa Mreno huyo amekubali kusaini miaka mitatu Old Trafford.

Lakini vyombo vya habari katika taarifa zake za jana, viliandika kuwa kama Van Gaal atashindwa kupata moja kati ya nafasi nne za juu kwenye msimamo, basi uwezekano wa Mourinho kuchukua timu utakuwa mkubwa.

United ilimtimua kazi Kocha David Moyes saa 36 baada ya Man United kufungwa 2-0 na Everton na hesabu kuonyesha kuwa timu hiyo isingeweza kumaliza miongoni mwa timu nne za juu.

Watu wa karibu wa Mourinho wanadai kuwa kocha huyo pamoja na kutaka nafasi United, lakini hafurahishwi na jinsi Van Gaal anavyoandamwa kutokana na kupata matokeo yasiyotarajiwa. Makocha hao wamekuwa karibu kwa miaka 16 sasa.

"Yeye ni mtu muhimu sana, lakini muhimu sana kwangu na tunaendelea na uhusiano wetu mzuri," aliwahi kukaririwa Van Gaal wakati akimzungumzia Mourinho msimu uliopita.

Kocha aliyepata mafanikio makubwa Old Trafford, Alex Ferguson hakusumbuka kumfanya Mourinho kuwa mbadala wake pale alipoamua kustaafu mwaka 2013 na bado anadaiwa kusisitiza kuwa kocha huyo Mreno siyo mtu sahihi kufundisha Mashetani Wekundu hao.

Habari Kubwa