Mshindi Maalim Seif CUP apatikana

23Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Pemba
Nipashe
Mshindi Maalim Seif CUP apatikana

TIMU kutoka Wete Kaskazini Pemba imenyakua ubingwa wa Kombe la Maalim Seif linalojulikana kama 'Maalim Seif CUP' katika fainali iliyochezwa jana, Oktoba 22,2021 kwenye Uwanja wa Madungu Polisi Chakechake Pemba.

Makamo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Khadija Anwar Mohamed akikabidhi kombe kwa Kapteni wa Timu ya Wete, Said Mohamed baada ya kuchukua ubingwa wa Kombe la Maalim Seif CUP ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanasiasa mashuhuri nchini, Maalim Seif Sharif Hamad Oktoba 22,2021.

Mashindano hayo maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa nguli wa siasa Zanzibar na Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad yalishirikisha timu 18 zote kutoka Pemba.

Miongoni mwake Timu kutoka Wete Kaskazini na Mkoa wa Kusini Pemba ziliingia fainali na Timu ya Wete Kaskazini ikaibuka kidedea na kujinyakulia zawadi ya kombe, jezi pea tatu na mipira miwili.

Mshindi wa pili Timu ya Mkoa wa Kusini Pemba na mkoa wa kichama Mkoani ilipata zawadi ya jezi pea mbili na mipira miwili.

Mshindi wa tatu alitokea Chake Chake huku mshindi wa nne akitokea Jimbo la Chambani ambayo ilipata zawadi ya jezi na mpira.

Akikabidhi zawadi kwa washiriki na washindi wa michuano hiyo, Makamo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Zanzibar, Khadija Anwar Mohammed alisema Mashindano hayo niya kwanza kufanyika baada ya kifo cha Marehemu Maalim Seif kufariki Dunia mapema mwaka huu.

Khadija ambaye pia alikuwa mgen rasmi katika fainali hizo, alisema timu zote 18 zilizoshiliki mashindano hayo zimepata zawadi ya mpira mmoja mmoja.

"Madhumuni makuu ya shughuli hii ya leo ni kukumbuka Siku ya kuzaliwa kwa Kiongozi wetu kipenzi cha Wazanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwaunganisha vijana jamii kwa ujumla wake.

Tunaahidi kuendelea kuenzi siku hii kila mwaka kwakuwa hii ni siku kubwa na maalum kwetu.

"Shukrani zangu nakwa niaba ya Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo tunawashukuru timu zote zilizoshiriki, wanachama pamoja na wote waliounga mkono mashindano haya" alisema Khadija.

Maalim Seif ambaye alitokea kuwa mwamba wa siasa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla alizaliwa Oktoba 22,mwaka 1943 na kufariki dunia Februari 17,2021.

Habari Kubwa