Mshindi wa pili Ligi Kuu sasa kucheza CAF

17Sep 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mshindi wa pili Ligi Kuu sasa kucheza CAF

BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imerekebisha baadhi ya kanuni msimu huu, na sasa mshindi wa pili wa ligi atacheza michuano ya Shirikisho barani Afrika (CAF), kama bingwa wa Ligi Kuu ndiye atakayetwaa pia Kombe la FA.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almas Kasongo, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, pamoja na kanuni nyingine zilizorekebishwa, kanuni hiyo imepitishwa, ili kuipa thamani Ligi Kuu, lakini pia kuleta ushindani kwenye michuano ya Kombe la FA.

"Tulitoa nafasi kwa wadau wote wa michezo kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni, na moja ya mabadiliko hayo ni kurekebisha hii ya mshindi wa pili wa Ligi Kuu, kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, kama ikitokea bingwa wa Ligi Kuu akachukua tena Kombe la FA," alisema Kasongo.

Alisema kanuni hii imerekebishwa, ili kuleta ushindani kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA pia.

Alisema baada ya kutafakari na kuangalia yaliyotokea, hasa kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA, Simba ikicheza dhidi ya Namungo, wakati tayari zote zikiwa zimeshakata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, kanuni hiyo ilionekana inahitajika.

Kutokana na mabadiliko hayo, timu yoyote sasa itakayofika fainali ya Kombe la FA na ikafungwa na timu ambayo pia imetwaa ubingwa, haitoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kama ilivyokuwa kwa Namungo mwaka huu dhidi ya Simba, badala yake timu itakayoshika nafasi ya pili kwenye ligi tu ndiyo itakayoshiriki michuano hiyo.

Hata hivyo, bingwa wa Kombe la FA bado ataendelea kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 Ikumbukuwe kuwa, bingwa wa Tanzania anaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hata ikitwaa tena Kombe la FA haiwezi kushiriki michuano hiyo.

Habari Kubwa