Msimbazi: Hesabu kwa Azam kwanza

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Msimbazi: Hesabu kwa Azam kwanza

SIKU moja baada ya kufanikiwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja,

Amesema ushindi huo ni salamu kwa Wanajangwani hao kuelekea kwenye mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Februari 18, mwaka huu, lakini kwa sasa wanaipigia hesabu Azam kwanza.

Mayanja akizungumza na gazeti hili jana, alisema timu yake ilistahili ushindi ndani ya dakika 90 za mchezo huo uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

"Ushindi dhidi ya Yanga hatukubahatisha, lakini pia nawasifu walijitahidi kwa sababu tulipanga kushinda ndani ya dakika 90, najua tutakutana nao tena kwenye ligi bado tunauwezo wa kuwafunga na huko," alisema Mayanja.

Aidha, alisema kwa sasa wanajiandaa na mchezo wao wa fainali dhidi ya Azam utakaochezwa kesho kwenye Uwanja huo wa Amaan.

Alisema mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani, lakini bado anaipa nafasi timu yake kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

"Azam ni timu nzuri na kwenye mashindano haya imeonekana kuwa na morali ya juu, tunategemea mchezo utakuwa mgumu na upinzani utakuwapo..., hata hivyo naamini Simba itafanya vizuri na kutwaa ubingwa," alisema Mayanja.

Alisema wameifuatilia Azam kwenye michezo yao na kocha mkuu (Joseph Omog) anajua nini cha kufanya kuelekea mechi hiyo ya fainali.

Fainali hiyo ya kesho itakuwa ya sita kwa upande wa Simba ambayo imetwaa ubingwa mara tatu wa michuano hiyo na kuwa timu iliyobeba kombe hilo mara nyingi zaidi tangu kuanzishwa kwake.

Azam wanashikana nafasi ya pili kwa kuchukua ubingwa huo mara mbili katika fainali mbili walizoingia za mashindano hayo.

Habari Kubwa