Msuva aiokoa Stars

08Oct 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Msuva aiokoa Stars

ZIKICHEZA kibabe timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) na Malawi (The Flames) zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.

Ngambi Robert ndiye aliyefunga bao kwa upande wa Malawi katika dakika ya 35 akipiga mpira mrefu uliomshinda kipa Aishi Manula kuudaka.

Taifa Stars ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Simon Msuva ambaye alipiga krosi iliyotinga moja kwa moja wavuni na kumshinda kipa wa Malawi kudaka katika dakika ya 57.

Malawi ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 na wachezaji wake wakionekana na "njaa" zaidi ya kusaka mabao zaidi.

Hata hivyo, Stars itajilaumu kupoteza nafasi tatu za kufunga katika dakika ya pili, tatu, 14 na 29 kupitia kwa mshambuliaji wake anayecheza soka la kulipwa Morocco, Msuva, kupiga mashuti yaliyoishia kudakwa na kipa wa Malawi, Swini Charles.

Dakika ya 55, Mbwana Samatta alikaribia kuipatia Stas bao la kusawazisha, lakini mpira wa kichwa alioupiga uliokolewa na beki wa Malawi na dakika iliyofuata kipa Swini alipangua mpira wa kona uliopigwa na Msuva na kulilinda lango lake.

Samatta alikaribia tena kuipatia Stars bao, lakini shuti alilopiga baada ya kupokea krosi ya Erasto Nyoni liligonga mwamba wa juu na kuokolewa na kipa wa Malawi Swini katika dakika ya 65.

KOCHA AONDOLEWA
Dakika ya 79 mpira ulilazimika kusimama kwa dakika mbili baada ya Kocha Mkuu wa Malawi, Ron van Geneugden kugoma kutoka kwenye benchi na kuja jukwaani kama alivyotakiwa na refa Israel Nkongo baada ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.

Kamisaa wa mechi hiyo, Leslie Liunda, alilazimika kushuka chini kwenda kumuondoa kocha Geneugden ili kuruhusu mpira uendelee.

Nkongo alimwonyesha Nyoni kadi nyekundu baada ya kumkanyaga mchezaji wa Malawi, Richard Mbulu ambaye ndiye alianza kumfanyia faulo kama hiyo kabla ya Mzamiru Yasin naye kuonyeshwa nyekundu dakika ya 90.

Taifa Stars: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Himid Mao, Simon Msuva /Abdul Hilal (dk. 83), Hamisi Abdallah/ Mzamiru Yassin (dk. 11), Mbwana Samatta, Raphael Daudi/ Mbaraka Yusuph (dk. 54) na Shiza Kichuya/Ibrahim Ajib (dk. 58).

Malawi: Swini Charles, Gomezgan Chirwa, Lanjesi John Chembezi Dennis. Fodya Nyamkuni, Ngambi Robert, Phiri Gerald, Banda John, Chirwa Kikoti, Mhango Gabadinho na Mbulu Richard.