Msuva atamani kumfuata Messi

03Aug 2017
Somoe Ng'itu
Dar es salaam
Nipashe
Msuva atamani kumfuata Messi

BAADA ya kuanza kufungua akaunti ya mabao katika klabu yake mpya ya Difaa El Jadida ya Morocco, mshambuliaji Simon Msuva, amesema anatamani kupata nafasi ya kusajiliwa na timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga, anapocheza mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Msuva, alisema kuwa anaamini La Liga ndiyo ligi bora duniani na ndoto yake inaweza kutimia kutokana na juhudi ambazo amejipanga kuzionyesha.

Msuva alisema kuwa kama asingekomaa msimu uliopita kwa kucheza kwa nguvu kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa waliyoshiriki, nafasi ya kuonekana na klabu za nje isingepatikana.

"Yanga ilikuwa katika wakati mgumu msimu uliopita, tumepita katika changamoto ambayo haijawahi kutokea kwa miaka minne iliyopita, lakini mimi niliweka mawazo pembeni na kusema nicheze kwa bidii ili malengo yangu yatimie," alisema Msuva.

Aliongeza kuwa nidhamu ya kusikiliza mafunzo uwanjani na nje ni moja ya vitu vilivyosaidia kumfikisha hapo na amewataka wachezaji wenzake wasibweteke na hatua waliyonayo sasa.

"Angalia hata kina Ngoma (Donald) wamekuja Yanga, lakini malengo yao ni kwenda Ulaya, na sisi wachezaji wa Tanzania tunaweza kutoka nje, ila kwanza ni lazima mchezaji uwe na malengo na uyaonyeshe kwa vitendo," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Moro United.

Aliwataka wachezaji wote kuendelea kujituma na kwake hatafikiria kurejea nchini kama ilivyotokea kwa baadhi ya nyota waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu Bara.

Habari Kubwa