Mtanzania aibuka mshindi Mumbai Marathon

16Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mtanzania aibuka mshindi Mumbai Marathon

MTANZANIA Alphonce Simbu, ameibuka mshindi wa mbio za Mumbai Marathon za mwaka huu akimpiku Mkenya Joshua Kipkorir pamoja na wanariadha wengine wazoefu.

MTANZANIA Alphonce Simbu.

Mashindano hayo yanajulikana kama 'Standard Chartered Mumbai Marathon' yanafanyika kila mwaka Jumapili ya tatu ya mwezi Januari katika Jiji la Mumbai, India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kutokana na idadi ya washiriki wanaomaliza mbio hizo.

Simbu, anayedhaminiwa na Kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa saa 2:09:28.

Akizungumzia ushindi wake, Simbu alisema kuwa anaamini ushindi huo umesababishwa na maandalizi aliyoyafanya.
Alisema anauchukulia ushindi huo kama changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu.

"Ushindi huu si wangu peke yangu, si wa Multichoice wadhamini wangu, ushindi huu ni wa Watazania wote," alisema Simbu.

Kwa upande wa Serikali, Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema , " "Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania."

Aidha, kwa upande wake, Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana, alisema Multichoice imefurahishwa sana na ushindi huo na wataendelea kumdhamini mwanariadha huyo.

“Tulichukua jukumu la kumdhamini Simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote, dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani,” alisema Mshana.

Simbu anatarajiwa kurejea nchini leo Jumatatu.

Habari Kubwa