Mtanzania ashinda marathon China

06Mar 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe Jumapili
Mtanzania ashinda marathon China

MWANARIADHA wa Tanzania Emmanuel Giniki anayefanya mazoezi katika taasisi ya michezo ya Shahanga (SSI) iliyopo Hanang’ mkoani Manyara, ameibuka mshindi wa mbio za Marathon za Kunming nchini China, akiwashinda washindani wake wa karibu kutoka Kenya na Ethiopia.

MWANARIADHA wa Tanzania Emmanuel Giniki

Giniki ameliambia gazeti hili kwa njia ya mtandao kutoka China kuwa mbio hizo za kilomita 21.1 zilifanyika Februari 28, mwaka huu na alishinda baada ya kutumia saa 01:03:50.

Kwa mujibu wa Giniki, nafasi ya pili ilishinkwa na Mkenya, Kiptoo Kibet, huku nafasi ya tatu ikienda kwa mwanariadha wa Ethiopia, Tsegaye Getachew Tadese.

Rekodi za mashindano ya mchezo wa riadha sehemu mbalimbali za dunia, ikiwamo ndani ya nchi, zinaonyesha wanariadha wa Kenya na Ethiopia kufanya vizuri zaidi ya Watanzania.

Giniki alisema pamoja na mashindano hayo kuandaliwa na mamlaka ya Mji Kunming, lakini yanawashirikisha wanariadha wa kimataifa kutoka nchi zaidi ya 20 duniani.

Mashindano hayo yalianza mwaka 1994, lakini Tanzania ilipata mshiriki wa kwanza, Ipyana Mwakabana mwaka 2001 ambaye hata hivyo hakufanya vizuri.Mtanzania mwingine, Joseph Panga alishiriki mbio hizo mwaka jana na kumaliza katika nafasi ya saba.

Kwa mujibu wa Giniki, hali kama hiyo ilitokea kwa wanariadha wanawake wa Tanzania, Fadhila Samwe na Natalia Elisante walioshika nafasi za nane na 14.

Kocha wa Giniki, Gidamis Shahanga wa SSI alisema ushindi huo ni mwendelezo mzuri wa mwanaridha Giniki anayesema anafungua njia ya kurejesha hadhi ya mchezo huo nchini.

Habari Kubwa