Mtibwa kambini leo mzunguko wa pili

20Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mtibwa kambini leo mzunguko wa pili

MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mtibwa Sugar wanatarajiwa kuingia kambini leo Manungu, Turiani mkoani Morogoro kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema jana mjini Dar es Salaam kuwa wachezaji wote na wafanyakazi wengine wa timu wataingia kambini Jumapili kwa maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

“Tunakutana Jumapili Saa 7:30 mchana kwa safari ya Manungu kwenda kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu katika kambi yetu ya Manungu,”alisema Bayser.

Mtibwa Sugar ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu katika nafasi ya tano kutokana na pointi 23 ilizokusanya katika mechi 15.

Bayser alisema timu haikumaliza katika nafasi mbaya, lakini malengo yalikuwa ni kumaliza juu zaidi. “Kwa kweli Mtibwa Sugar tulikuwa na malengo ya kushika nafasi nne za juu, katika mzunguko wa kwanza na badala yake tumeshika ya tano katika msimamo,”alisema.

“Na hii imesababishwa na mambo makuu mawili, kwanza msimu huu tuliondokewa na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza, hivyo basi mwalimu anajaribu kutengeneza kikosi kipya kutokana na wachezaji waliopo na waliosajiliwa na sababu nyingine ni kuwa tumebadilisha kocha mkuu na analeta mfumo wake na aina yake ya uchezaji,”aliongeza.

Habari Kubwa