Mtibwa sasa yajikita kwenye usajili

26Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mtibwa sasa yajikita kwenye usajili

BAADA ya kufanikiwa kubaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mohammed Badru, amesema yuko makini katika usajili wa wachezaji na kufanya maandalizi mazuri kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mtibwa Sugar imefanikiwa kubaki katika ligi, baada ya kupata matokeo mazuri katika michezo yake miwili ya Play Off kwa kumfunga Transit Cape FC.

Akizungumza na gazeti hili jana, Badru alisema atakabidhi ripoti yake itakayoeleza nafasi anazotaka kusajili kwa lengo la kuboresha kikosi chake kuelekea msimu.

Alisema alipofika Mtibwa Sugar ni mwishoni mwa msimu na kufanikiwa kuibakiza katika ligi sasa anahitaji kuimarisha kwa kufanya usajili kulingana na mahitaji ya timu yake na kufanya vizuri kwa msimu ujao.

"Msimu huu ulioisha haukuwa mzuri kwa Mtibwa Sugar, tumeona upungufu, nina imani tunafanyia kazi pungufu wetu ikiwamo usajili wa wachezaji wapya na kuwapandisha wachezaji kutoka kikosi cha vijana," alisema.

Alisema anafurahi wachezaji wamepambana katika michezo miwili ya Play off na kuendelea kubaki katika ligi hiyo kwa msimu ujao na kuhakikisha makosa yaliyojitokeza msimu huu, kutojirudia kwa msimu ujao.