Mtibwa Sugar yajitosa kumwania nyota Yanga

05Aug 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mtibwa Sugar yajitosa kumwania nyota Yanga

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umeonyesha nia ya kutaka kumsajili beki wa kulia wa Yanga, Said Makapu kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la FA.

Makapu pia ana uwezo wa kucheza kwa ufasaha nafasi ya kiungo mkabaji, beki ya kati na kulia, amekuwa hana namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mohammed Badru alisema katika ripoti amependekeza nafasi za wachezaji anaotaka wasajiliwe, pia alitaja majina ya nyota anaowahitaji kama watapatikana.

Hata hivyo Badru hakuwa tayari kusema kama wameshaanza mazungumzo na Makapu.

Badru alisema anahitaji kusajili wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kukabiliana na ushindani uliopo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na hataki kuona kikosi chake kinakuwa wasindikizaji.

Kocha huyo alisema hawezi kuweka wazi majina ya wachezaji wengine kwa sababu kuna wengine wanawindwa na timu nyingine, hivyo zinaweza kuongeza ushindani.

"Kuna wachezaji nimewataja majina, kwa sasa siwezi kuweka wazi majina hayo, ila tusubiri viongozi wafanyie kazi ripoti yangu kama nilivyopendekeza, ninahitaji beki wa kuli, beki wa kati na kiungo mkabaji," alisema Badru.

Aliongeza msimu uliopita walimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa presha, hivyo wanajipanga kujiimarisha kwa kufanya usajili makini, ili makosa yaliyojitokeza yasijirudie.

"Hatutaki kujiweka katika presha kubwa kama ilivyokuwa msimu uliopita, hatutaki kurudia makosa yale yale, tumejipanga kufanya vizuri katika michezo yote ya ligi na Kombe la FA," Badru alisema.

Aliongeza anafahamu kila timu iko kwenye mchakato wa kuimarisha kikosi chake na wao wanahitaji kukamilisha malengo yao mapema na kuanza maandalizi ya msimu mpya kama walivyopanga.

"Ni kweli Makupu ni miongoni mwa wachezaji walioorodheshwa katika ripoti ya Kocha Bandru, kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu yetu kwa msimu mpya wa Ligi Kuu, tunafanyia kazi kuona kama tutampata maana kuna ofa kutoka timu nyingine zinamhitaji," kilisema chanzo chetu.