Mtibwa yakubali mambo magumu

01Jul 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mtibwa yakubali mambo magumu

KLABU ya Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza imekiri iko katika hali ngumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na inatakiwa 'ikaze msuli' ili ijiondoe kwenye janga la kushuka daraja.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru:PICHA NA MTANDAO

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru, alisema jana msimu huu haukuwa mzuri kwao, lakini watajitahidi kwa kila hali, wakiwa na wachezaji wazuri pamoja na benchi la ufundi, hata hivyo imeshindikana na badala yake wamejikuta wakiwa kwenye hali hiyo.

"Tupo kwenye hali ngumu sana, miaka 25 tumekuwa kwenye ligi, lakini sitousahau mwaka huu au msimu huu wa 2019/20, tunapitia kipindi kigumu sana na hatujawahi kushika nafasi za chini kama hizi, lakini kuomba Mungu ili tusalie Ligi Kuu na tukifanikiwa, tutaanza kufanya marekebisho ya kikosi kwa msimu ujao," alisema Kifaru.

Alitangaza rasmi kuwa iwapo Mtibwa Sugar itashuka daraja, basi atastaafu nafasi yake katika klabu hiyo ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

"Kama itatokea bahati mbaya tukishuka, basi na mimi nitastaafu kazi hii, lakini kwa sasa tuna mechi mbili ngumu za ugenini huko Mwanza dhidi ya Alliance na Mbao, tutajitahidi kupata ushindi kwenye mechi hizi ili tuwe kwenye hali nzuri," Kifaru alisema.

Mtibwa iko katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 32, imeshinda mechi tisa, sare 10 na kufungwa mechi 13.

Habari Kubwa