Mtunisia wa Yanga na mkakati wa kibingwa

21Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mtunisia wa Yanga na mkakati wa kibingwa
  • ***Ashuka na wasaidizi wawili, ataka muda kuisuka upya huku akieleza anataka kuifanya kuwa...

KOCHA Mkuu wa Klabu Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi, ameeleza mikakati yake mizito ya kuifanyia klabu hiyo baada ya kutua nchini na kuingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu, ambapo sasa anachukua rasmi nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Mrundi Cedric Kaze, aliyetimuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nabi alisema anafurahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Yanga ambayo ni moja kati ya timu kubwa Afrika Mashariki na Kati na anataka kuhakikisha uwezo wake wa kufanya vizuri.

Alisema Yanga ina historia nzuri na ana imani ya kufanya vizuri hapo baadaye kwa sababu ya kulifahamu soka la Afrika.

"Nahitaji muda wa kuandaa timu, kiufundi pamoja na kuweka mipango yangu sawa kwa sababu nimekuja tayari timu iko mwishoni mwa msimu, nina imani kwa ushirikiano mzuri na uongozi tutafikia malengo yanayotarajiwa na Wanayanga," alisema Nabi.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa Klabu ya Al-Merrikh ya Sudan akichukua nafasi ya Mfaransa wa Simba, Didier Gomes, alifutwa kazi ndani ya klabu hiyo baada ya kutopata matokeo mazuri hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Kwa upande wa uongozi wa Yanga, ukizungumza na gazeti hili jijini jana kuhusu ujio wa Nabi, Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Hajji Mfikirwa, alisema kocha huyo amekuja na wasaidizi wake wawili, msaidizi ambaye ni Jawad Sabri na Sghir Hammadi ambaye ni kocha wa viungo.

Alisema wamechukuwa uamuzi huo wa kukubali aje na wasaidizi wake kwa sababu atakuwa na urahisi mkubwa wa kufanya kazi na watu ambao anawafahamu.

"Mpango wa kumleta Nabi kwa sasa ni kuhakikisha kocha huyo anapata muda wa kuona upungufu wa kikosi cha timu yetu kwa ajili ya kufanyia kazi msimu ujao.

"Ujio wa kocha huyo umezingatia pia ushiriki wetu wa michuano ya kimataifa kwa msimu ujao," alisema Mfikirwa.

Alisema kuhusu Kocha Juma Mwambusi, ataendelea kuwapo ndani ya benchi hilo la ufundi akimuelekeza Nabi hadi msimu ujao wataona ni sehemu gani anapaswa kuwapo.

Nabi alipata nafasi ya kuishuhudia timu yake hiyo mpya ikicheza dhidi ya Gwambina FC jana usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Habari Kubwa