Muuaji Simba alilia tuzo ya Kichuya

21Apr 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Muuaji Simba alilia tuzo ya Kichuya

MSHAMBULIAJI wa Toto Africans, Waziri Sentembo amesema kuwa anaamini kuwa alipaswa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Machi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, badala ya Shiza Kichuya.

Waziri Sentembo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mshambuliaji huyo maarufu kama Waziri Junior aliyefunga bao pekee dhidi ya Simba na kuifanya Toto kuibuka na ushindi wa bao 1-0 alisema licha ya kutoshinda, hakuingizwa hata kwenye kinyang'anyiro cha kuchuana kuwania kuchaguliwa kutokana na kuisaidia timu yake ya Toto kwenye mechi kadhaa mwezi Machi.

"Nimesikitika sana kuikosa tuzo ya uchezaji bora wa mwezi, niliamini kuwa ni mimi ndiye niliyepaswa kuchaguliwa, lakini amechaguliwa mchezaji mwingine," alisema na kuongeza:

"Sijui ni nini, lakini nadhani kuna vitu kanizidi, sina tatizo naye nampongeza, lakini naamini tena naweza kuchukua uchezaji bora Aprili," alisema Waziri ambaye kwa sasa ana magoli saba ya kufunga.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kichuya alionyesha kiwango cha juu Machi katika raundi ya nne ya ligi na kuisaidia timu yake kushinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza.

Katika mechi hizo ambazo zote Kichuya alicheza, alifanikiwa kufunga mabao mawili kati ya matano yaliyofungwa na timu yake.

Alifunga dhidi ya Coastal Union kwa ushindi wa mabao 3-0, na JKT Ruvu Stars na dhidi ya Mtibwa Sugar iliyoshinda mabao 2-1.

Hata hivyo kwa mujibu wa rekodi za Nipashe, Machi ilifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar.

Kwa upande wa Waziri, pia amefunga magoli mawili moja timu yake ikishinda ugenini mabao 2-1 dhidi ya African Sports, lingine akiisawazishia Toto na kutoka bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Machi hiyohiyo, Toto ilipoteza mechi mbili, ilipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Mgambo Shooting na 2-0 dhidi ya JKT Ruvu.

Habari Kubwa